Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mhe. Anne Makinda akisaini kitabu cha Wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma wakati wa hafla za uzinduzi wa kampeni za kuhamasisha wananchi kujiunga na vifurushi vya Bima ya Afya, leo mkoani Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali (Mstf) Emmanuel Maganga akimueleza jambo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mhe. Anne Makinda wakati wa hafla za uzinduzi wa kampeni za kuhamasisha wananchi kujiunga na vifurushi vya Bima ya Afya.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga akiongea na wakazi wa Kigoma wakati wa hafla za uzinduzi wa kampeni za kuhamasisha wananchi kujiunga na vifurushi vya Bima ya Afya, ambapo alisema mnufaika wa vifurushi hivi atapata huduma kuanzia ngazi ya zahanati mpaka taifa kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa, leo mkoani Kigoma
Mwenyekti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma za Maendeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba akiongea na wakazi wa Kigoma wakati wa hafla za uzinduzi wa kampeni za kuhamasisha wananchi kujiunga na vifurushi vya Bima ya Afya, ambapo alisema kuwa Ukiona mwanasiasa anapinga vifurushi, ujue huyo ni mwanasiasa uchwara, huyo ni mwanasiasa ambaye haendi hospitali kuona watu wanavyopata shida, leo mkoani Kigoma
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mhe. Anne Makinda, akiongea na wakazi wa Kigoma wakati wa hafla za uzinduzi wa kampeni za kuhamasisha wananchi kujiunga na vifurushi vya Bima ya Afya ambapo alisema kuwa bila bima hauna maisha, gharama za matibabu kwa sasa ni kubwa sana, Bima inakufanya uwe salama, Bima ni mlinzi kwako na familia yako, leo mkoani Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali (Mstf) Emmanuel Maganga , akiongea na wakazi wa Kigoma wakati wa hafla za uzinduzi wa kampeni za kuhamasisha wananchi kujiunga na vifurushi vya Bima ya Afya, ambapo alisema kuwa mpango wa vifurushi vya bima ya afya ni mfumo bora ambao umejaribiwa duniani unaotumiwa kwa ajili matibabu na kuwataka viongozi wa Mkoa kwenda nyumba kwa nyumba kuhakikisha wananchi wanajiunga na mpango huu wa vifurushi
Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla za uzinduzi wa kampeni za kuhamasisha wananchi kujiunga na vifurushi vya Bima ya Afya.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali (Mstf) Emmanuel Maganga na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mhe. Anne Makinda wakiwa katika picha ya pamoja na wakazi wa Kigoma waliokata Bima ya Afya kupitia mfumo wa Vifurushi.
PICHA NA IDARA YA HABARI-MAELEZO
………………
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Wakazi wa Mkoa wa Kigoma wamesema kuwa mpango wa Vifurushi vya Bima ya Afya ni mpango mzuri unaolenga kuwakomboa wananchi kwa kuwahakikishia upatikanaji wa huduma za matibabu wakati wowote wanapopatwa na magonjwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa halfa ya uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiunga na vifurushi vya Bima ya Afya Mkoani Kigoma , wakati hao wamesema kuwa mpango wa vifurushi unampa mwananchi fursa ya kuchagua huduma anazotaka kwa gharama nafuuu na kuwa na uhakika wa kupata matibabu katika mkoa wowote nchini.
Mkazi wa maeneo ya Mwanga Bw. Nobert Makofi alisema kuwa awali hakuona umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya lakini kwa mpango huu amechukua hatua za kujiunga na kuahidi kuwa balozi wa uhamasishaji wa wananchi wengine kujiunga na huduma hiyo.
“Najitolea kuwa balozi wa kuhamasisha wananchi wenzangu wajiunge, kuna hatari kubwa ya mwananchi kuishi bila kuwa na uhakika wa kupata matibabu kupitia bima ya afya, wengi tunapoteza maisha kutokana na kukosa fedha za kugharamia matibabu lakini mpango huu unatupa fursa kubwa ya kujikinga afya zetu kwa kujiunga na kifurushi,” alisema Bw. Makofi.
Mwanachama mwingine Bi. Tausi Kitumbo ambaye amepokea kadi yake wakati wa uzinduzi ametoa wito kwa akina mama kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii kujiunga na vifurushi hivyo ili kuhakikisha familia zao zinakuwa na uhakika wa matibabu wakati wowote.
“Mwanamke ndio mwangalizi wa familia hivyo kama mama ni vyema ukawa mstari wa mbele kuhakikisha familia yako unailinda kwa kuikatia kifurushi chochote na gharama hii inawezekana hata kama kwa kuweka fedha kidogo kidogo,” alisema Bi. Tausi.
Aidha, Bi Tausi Saidi amesema kuwa hakuwa amejiunga na mpango wa vifurushi ila kutokana na hamasa aliyoipata katika uzinduzi wa kampeni hizi atahakikisha anajiunga na mpango huu kutokana na umuhimu wake kwa afya yake na anauhakika atakata na kuwa balozi wa mpango huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Huduma za Maendeleo ya Jamii, Mhe. Peter Serukamba alisema kuwa suala la afya sio la mchezo na ukikutana na mwanasiasa anayefanya upotoshaji kwenye afya huyo ni mwanasia uchwara na ambaye hatembelei wagonjwa hospitali na kuona wanavyopata shida.
Akizindua mpango wa uhamasishaji Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga aliagiza viongozi wote mkoani humo kuhakikisha wanasimamia suala hilo kwa kufanya kampeni ya nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa na wanachukua hatua ya kujiunga.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unaendelea na uhamasishaji wa wananchi kujiunga na mpango wa vifurushi vipya ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.