Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kwenye Ufunguzi wa Kongamano la Bima ya Afya kwa Wote na Jukwaa la Kitaifa la Majadiliano ya Ugharamiaji wa Huduma za Afya, kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa AICC jijini Arusha Oktoba 30, 2024 wakati alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kongamano hilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Washirika wa Maendeleo kushikiriana na Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na kusaidia kuimarisha mfumo wa ugharamiaji huduma za afya ili kuufanya kuwa endelevu.
Mheshimiwa Majaliwa amesema ili kuimarisha mfumo wa ugharimiaji wa huduma za afya Serikali tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuendelea kuongeza kiwango cha bajeti ya Sekta ya Afya.
Ametoa wito huo leo (Jumatano Oktoba 30, 2024) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa mdahalo wa Bima ya Afya kwa Wote na Jukwaa la Kitaifa la Ugharamiaji wa Huduma za Afya kwa ajili ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (Universal Health Insurance – UHI), jijini Arusha.
“Pia, tumeanzisha mfuko kwa ajili ya kugharimia wananchi wasio na uwezo, tumebainisha vyanzo mahsusi vya fedha kwa ajili ya kugharimia Bima ya Afya kwa wananchi wasio na uwezo ambapo katika bajeti ya mwaka 2024/2025 zimetengwa shilingi bilioni 173.5 kwa madhumuni hayo.”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utafanikiwa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa miundombinu na uborashaji wa huduma za uchunguzi.
Amesema Serikali imewekeza katika ununuzi na usimikaji wa vifaa tiba vya kisasa vya uchunguzi na ugunduzi wa magonjwa mbalimbali, ambapo hadi sasa zipo mashine za MRI 13, CT-Scan 45, Digital X-Ray 346 na Ultrasound 668 kutoka 476 zilizokuwepo mwaka 2021. “Hatua hii imewezesha kupatikana kwa huduma za kibingwa za uchunguzi.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imeendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa nchini kwa kutoa fedha kila mwezi kwa ajili ya ununuzi wa dawa.
“Hadi kufikia Oktoba 2024 upatikanaji ulikuwa umefikia wastani wa asilimia 85 ambapo kwa upande wa zahanati ni asilimia 76, vituo cha afya ni asilimia 75, Hospitali za Halmashauri asilimia ni 78, Hospitali za Rufaa za Mikoa ni asilimia 99 na Hospitali ya Taifa, Maalum na kanda ni asilimia 98”.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya Jenista Mhagama amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza sana kwenye sekta ya afya kwa kuwa anatambua afya ni usalama, ulinzi wa Taifa na ni maendeleo ya Taifa.
Amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya Sita, sekta ya afya imeendelea kupewa kipaumbele kwa kutengewa jumla ya shilingi trilioni 6.2 kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali zilizomwezesha mwananchi kupata huduma bora za afya karibu na maeneo yao.
“Haya ni maamuzi ya kizalendo kwa muktadha wa Taifa letu katika kutekeleza maono ya Baba wa Taifa ya kupambana na maadui wa umaskini (maradhi).”
Naye, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani, Dkt. Charles Sagoe-Moses amesema Shirika hilo linaahidi kusaidia utekelezaji wa Mpango Bima ya Afya kwa Wote lengo likiwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa.
Aidha, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira ya dhati ya kuanzisha mchakato wa Kitaifa wa Bima ya Afya kwa wote kama nyenzo ya kufikia huduma za afya kwa wote.
“Utekelezaji wa Bima ya Afya ya Wote, sio tu utakuwa na faida kwa afya ya Watanzania, bali itaacha alama katika uongozi wake Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya.”
Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Washirika wa Maendeleo nchini Tanzania, Moustafa Abdallah amesema kuwa watajitoa kusaidia safari ya Tanzania katika utekelezaji wa mpango huo ili kuwawezesha Watanzania kupata huduma bora za afya bila kujali uwezo wao wa kijamii na kiuchumi.
“Kwa kufanya kazi pamoja kati ya Serikali, washirika wa maendeleo, watendaji wa sekta binafsi na wadau wote, tunaweza kuhakikisha kuwa bima ya afya kwa wote inakuwa kweli, na kuwahakikishia Watanzania wote afya bora.”