Bungeni, Dodoma
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amelieleza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu manufaa yaliyopatikana kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya na vijiji vinavyozunguka Kiwanda cha Kuzalisha Gesi ya Ukaa (Carbon Dioxide) kuwa ni pamoja na malipo ya kiasi cha Shilingi Milioni 213 kama ushuru wa huduma katika kipindi cha kuanzia Januari 2020 hadi Oktoba 2023.
Dkt. Kiruswa ameyasema hayo leo Oktoba 29, 2024 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Sophia Mwakagenda Mbunge wa Viti Maalum aliyetaka kujua manufaa vinavyopata vijiji hivyo kutokana na uwepo wa kiwanda hicho.
Ameongeza kwamba, kiwanda hicho kinachomilikiwa na Kampuni ya TOL Gasses Limited, kimechangia kiasi cha Shilingi Milioni 159 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Isebe, vyumba viwili vya madarasa, pamoja na Ofisi ya Shule ya Sekondari Itagata, ujenzi wa uzio katika Shule ya Msingi Katumba, na ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa darasa katika Shule ya Sekondari ya Itagata, pamoja na Ofisi ya Kijiji;
‘’Mhe Spika, mbali na hayo, kiwanda hicho kimetoa ajira za kudumu 112 na ajira za muda mfupi takribani 150 kwa wananchi wanaotoka maeneo yaliyo jirani na kiwanda kama sehemu ya uwajibikaji wao kwa jamii kwa mujibu wa Kanuni za Uwajibikaji wa kampuni za Uchimbaji madini kwa Jamii (Corporate Social Responsibility – CSR),’’ amesema Dkt. Kiruswa.
Amefafanua kuwa, kutokana na leseni ya madini ya mradi huo kuwa katika Halmashauri za Wilaya za Rungwe na Busokelo, mwaka 2024 kampuni ya TOL Gasese Limited iliwekeana mkataba na Halmashauri ya Busokelo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mabweni ya Shule ya Msingi Lupata kwa thamani ya Shilingi milioni 39.7 ambapo mradi huo umekamilika.
‘’ Mhe, Spika, vilevile kampuni ya TOL Gases inatarajia kukaa na Halmashauri zote mbili mwezi Desemba 2024 ili kuandaa na kuweka mpango wa utekelezaji wa CSR kwa mwaka 2025,’’ amesititiza Dkt. Kiruswa.