Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imesema inaandaa mkakati maalumu wa kuahikikisha muziki wa dansi haufi kwa kuendeleza bendi kongwe ambazo zimekuwepo muda mrefu ikiwemo bendi ya Msondo Ngoma.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro kwenye hafla ya Maadhimisho ya miaka 60 ya bendi kongwe ya Msondo Ngoma Oktoba 26, 2024 Jijini Dar es Salaam.
“Sisi kama Wizara yenye dhamana tunakuja na mkakati wa kuhakikisha muziki wa dansi haufi, tunakuja na mkakati wa kuhakikisha bendi zetu kongwe zinandelea kama ilivyo kwa timu kongwe za Simba na Yanga, tunataka Msondo na Sikinde zirudi kwenye hadhi yake” Amesema Mhe. Ndumbaro.
Mhe. Ndumbaro ameelekeza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuandaa mafunzo kwa viongozi wa bendi hizo ya jinsi ya kuendesha bendi kwa mtindo wa kisasa yatakayojumuisha wataalamu wa ndani na nje ya nchi.
Bendi ya Msondo inakumbukwa kwa nyimbo zake zenye maudhui ya kuelemisha, kuburudisha na kuhamasisha uzalendo kwa watanzania tangu ilipoanzishwa mwaka 1964.