Na Sophia Kingimali
Kutokana na mazingira wezeshi ya uwekezaji yanayotekelezwa nchini, Serikali imezitaka taasisi za umma kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kujiendesha kibiashara ili kuchangia ukuaji wa uchumi.
Akizungumza leo, Oktoba 25, 2024, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa pili wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na wadau wake jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, alisema mkutano huo ni ishara kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi na shirikishi kwa ajili ya uwekezaji na biashara nchini.
Kigahe alibainisha kuwa utoaji wa huduma kibiashara kwa taasisi za umma utachangia kuimarika kwa pato la taifa na kuwezesha kila mwananchi kupata huduma muhimu, zikiwemo za maendeleo.
“Tangu BRELA ianze kuandaa mikutano ya wadau, imefanikiwa kufanya maboresho ambayo yameongeza ufanisi na ubora wa huduma zake,” alisema Kigahe. “Taasisi nyingine za Serikali ambazo hazijaanza utaratibu huu zinapaswa kuiga mfano huu mzuri kwa kuwa unatoa fursa ya kupata maoni na mtazamo wa wadau badala ya kujitathmini wenyewe.”
Pia alisisitiza umuhimu wa BRELA kama lango la urasimishaji wa biashara, ikihusisha usajili wa kampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, na leseni za kitaifa na kimataifa, na kuifanya kuwa taasisi muhimu katika ujenzi wa taifa. Aliongeza kuwa mafanikio ya BRELA yanategemea ushirikiano kati ya sekta za umma na sekta binafsi.
“Mkutano huu unalenga kutathmini hatua zilizofikiwa na malengo ya baadaye katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo,” aliongeza.
Kigahe pia alisifu kaulimbiu ya mkutano huo, “Mifumo ya Kitaasisi Inayosomana na Uwezeshaji wa Biashara Nchini,” akisema inapaswa kujadiliwa kwa kina kwa kuwa mifumo hiyo inatakiwa kufanya kazi kwa pamoja ili kuimarisha utoaji wa huduma.
“Serikali imetoa maelekezo kuwa ifikapo Desemba mwaka huu, taasisi zote za umma ziwe na mifumo inayosomana ili kuondoa usumbufu na kero wakati wa kuwahudumia wananchi,” alisema.
Aidha, alieleza kuwa viongozi na maofisa kutoka nchi za Burundi, Sudan Kusini, na Kenya wamekuwa wakitembelea BRELA ili kujifunza mbinu za utoaji huduma kwa ufanisi kupitia mifumo.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, alisema mkutano huo unawashirikisha wawakilishi kutoka sekta za umma, taasisi na mashirika ya umma na binafsi, wawekezaji, na wafanyabiashara.
Nyaisa alisema kuwa mwaka 2015, BRELA ilianzisha mfumo wa kwanza wa usajili wa majina ya biashara kwa njia ya mtandao, mfumo uliotengenezwa na watumishi wa BRELA wakishirikiana na vijana wa Kitanzania, jambo linaloashiria uwezo wa vijana wanapopewa nafasi.
“Kwa sasa, BRELA inaendelea kuboresha mifumo yake kulingana na mahitaji,” alisema Nyaisa.
Mwenyekiti wa Bodi ya BRELA, Profesa Neema Molel, alisema bodi hiyo imeleta mafanikio makubwa ndani ya BRELA kwa kufanikisha dhima ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mifumo ya taasisi za serikali inasomana.
“Tumeweza kuchangia mfuko wa serikali kwa lengo la kutoa huduma bora kwa jamii, na mifumo ya BRELA imeweza kuunganishwa na taasisi nyingine za serikali ikiwemo TRA,” alisema Profesa Molel.