Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kimetoa vifaa kwa kwa vikundi vya wanawake na vijana wanaojishughulisha na kilimo cha Mwani ili waweze kuongeza thamani ya zao hilo na kukuza kipato chao.
Akikabidhi vifaa hivyo leo Jijini Dar es salaam Octoba 25, 2024 Mkurugenzi Mkazi wa UNDP Tanzania Shigeki Komatsubara amesema UNDP itaendelea kutoa msaada kwa wanawake na vijana wanaojishughulisha na kilimo cha mwani ili kukuza sekta ya uchumi wa bluu.
Aidha Vifaa hivyo ni ufadhili wa shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP) Tanzania katika utekelezaji wa mradi wa “Maisha Bahari” unaotekelezwa na chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini.
“Ufadhili wa vifaa hivi ni sehemu ya utekelezaji wa agenda ya kimataifa ya uchumi wa bluu,Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopiga hatua kubwa kwenye uchumi wa bluu katika sekta ya mwani “amesema Komatsubara
Kwa Upande wake, Dkt Edwin Mhede ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede amesema suala la kuchagiza maendeleo ya Uvuvi na Kilimo cha Mwani ni utekelezaji wa azimio namba 14 la Maendeleo endelevu ya Dunia, Ili ifikapo mwaka 2030 tuwe tumepiga hatua kwenye azimio namba 14.
“Nakipongeza chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini kwa kuwa mstari wa mbele kuchagiza na kuwa sehemu ya kutoa mafunzo kwa wakulima wetu ili kuhakikisha wanapata ufahamu wa matumizi sahihi ya teknolojia ili kuongeza thamani ya mwani na kukuza kipato cha Wakulima hawa”amesema Dkt Mhede
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dr. Batilda Burian amesema Mkoa wa Tanga una rasirimali za bahari na umekuwa ukitoa msisitizo katika kuhakikisha wanaimarisha usalama kwenye shughuli za uvuvi pamoja na kilimo cha Mwani.
Dr.Burian amesema kwa sasa Mkoa wa Tanga una wakulima wa mwani wapatao elfu Tano( 5,000 )na vikundi 20 vya wanenepeshaji wa kaa, pamoja na wafugaji wa jongoo bahari.
“Kitu tunachokifanya leo ni jambo ambalo linaweza kuchochea shughuli zetu za uchumi wa bluu,tunaona kuna fursa kubwa katika kilimo hiki japo tumeanza kwa kuchelewa wezentu wa Zanzibar walitagulia tangu miaka ya 2001 tayari wao walikuwa katika kilimo cha mwani”amesisitiza Dr.Burian
Nakuongeza kuwa lengo la Mkoa huo ni kukipeleka kilimo cha mwani mbali zaidi na kueleza kuwa wanafursa hiyo kutokana na kuwa na eneo la bahari lenye ukubwa wa kilometa 180 .
“Tunawashukuru UNDP kwa uwezeshaji huu walioufanya,kwanza wametoa mafunzo ya wakulima wetu wa mwani na vikundi mbalimbali kwa Mkoa wa Tanga zaidi ya wakulima 50 wamepata mafunzo sambamba na mashine za kusaga na kukausha mwani pamoja na kamba na Taitai “amesema
Awali Mkurugenzi wa chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kanda ya ziwa (Mwanza) Profesa Juvenal Nkonoki ambaye pia ni makamu Mkuu wa Chuo hicho amesema Mradi wa bahari maisha ni sehumu ya juhudi za kusaidia jamii za Pwani kupitia kilimo Cha mwani, ufugaji wa kaa, na ufugaji wa jongoo bahari.
“Kwa kutambua umuhimu wa mradi huu katika kuchangia uchumi wa jamii za Pwani na umelenga kuwawezesha wanawake na vijana waliopo katika mnyororo wa thamani wa rasilimali za bahari kupitia mradi wa bahari maisha”amesema Profesa Nkonoki
Nakuongeza kuwa “Tunaweka msukumo mpya wa kuongeza tija, kuongeza thamani ya mazao ya bahari na kulinda mazingira ya baharini kwa vizazi vijavyo”.
Aidha amesema utekelezaji wa mradi “BAHARI MAISHA” ulianza kwa hatua za awali kwa kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini chagamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa mwani , wafugaji wa kaa, na jongoo bahari chini ya wataalamu kutoka chuo cha mipango ya maendeleo vijijini kwa kushirikiana na UNDP Tanzania pamoja na mtaalamu kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam.
Profesa Nkonoki ameeleza kuwa wataalamu hao walitembelea maeneo manne ya mradi ambayo ni Tanga, bagamoyo, Ugunja na Pemba na kukutana na wakulima na wafugaji Ili kupata taarifa muhimu.
Amefafanua kuwa katika ziara hiyo waliweza kubaini chagamoto kadhaa kubwa ikiwemo uwezo mdogo wa wakulima na wafugaji katika kutumia mbinu bora za kilimo na ufugaji pamoja na ukosefu wa vifaa vya kisiasa kama vile kamba, Taitai, na mashine za kusaga mwani.
“Baada ya kubaini chagamoto hizo chuo cha mipango ya maendeleo vijijini kwa kushirikiana UNDP Tanzania tuliandaa programu ya mafunzo maalumu kwa wakulima wa mwani, wafugaji wa kaa, wafugaji wa jongoo bahari kutoka Ugunja, Pemba Tanga na bagamoyo”amesema
Vilevile amesema wanufaika wa mradi huo walipewa mafunzo ili kuwawezesha kuboresha uwezo wao katika maeneo muhimu kama vile kuwapatia mbinu bora za kilimo cha mwani, unenepeshaji wa kaa, ufugaji wa jongoo bahari na utunzaji wa kumbukumbu za fedha.
Wakizungumza na Fatma Makame kutoka Unguja ameiomba serikali kuliangalia upya suala la bei ya Mwani ili wakulima waweze kunufaika zaidi.
Kwa Upande wake, Suzana Mwita Kiongozi wa wanufaika hao kutoka Bagamoyo ameiomba serikali kuwajengea kiwanda cha kuchakata Mwani kwani uwezo wa kufanya hivyo wanao.