Na Ashrack Miraji, Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Jaffary Kubecha, amesema lengo la Kongamano la Samia Challenge, linalotarajiwa kufanyika kesho jijini Tanga, ni kupima uelewa wa vijana na watoto kuhusu maendeleo yaliyopatikana katika wilaya hiyo na mkoa wa Tanga kwa ujumla.
Kubecha alitoa kauli hiyo leo alipozungumza na waandishi wa habari, ambapo alibainisha kuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian, na litafanyika katika Ukumbi wa Samia Business Centre, Kange.
Ameeleza kuwa tayari wameweka matangazo kwenye shule na mitaani ili kuwahamasisha watoto kujitokeza kushiriki kongamano hilo litakaloanza saa mbili asubuhi. Aidha, alisisitiza kuwa mkoa wa Tanga una miradi mingi muhimu iliyotekelezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maslahi ya taifa.
“Maandalizi ya Kongamano hili yamekamilika, na tunalenga kuwashindanisha vijana na watoto wenye umri wa kati na chini ili kupima uelewa wao kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu, ikijumuisha sekta za elimu, afya, maji, na nishati ya umeme. Hasa ukizingatia kuwa zamani umeme ulikuwa unakatika mara kwa mara, lakini tangu nimefika sijashuhudia tatizo hilo,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali imefanya maboresho makubwa katika miundombinu, ikiwemo Bandari ya Tanga na Uwanja wa Ndege wa Tanga, ambapo wananchi wameanza kulipwa fidia kwa ajili ya kupisha upanuzi wa uwanja huo pamoja na miundombinu ya barabara na kuweka taa za barabarani katika maeneo mengi.
Kubecha pia alibainisha kuwa usalama umeimarishwa kupitia uwekaji wa kamera za usalama kwenye jiji la Tanga, na kwa hiyo ni muhimu kwa vijana na watoto kuelewa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa nchini chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.