Mfuko wa SELF unashiriki wiki ya huduma za Fedha yanayoendelea kwenye viwanja vya Luanda Nzovwe mkoani Mbeya kwa lengo la kutoa elimu kwa umma, hususan juu ya nidhamu ya mikopo na maswali muhimu ya kuuliza wakati wa kuomba mkopo ili kujiepusha na mikopo umiza maarufu kama ‘Kausha Damu’.
Akizungumza leo Oktoba 23, 2024, Meneja Masoko na Uhamasishaji wa Mfuko wa SELF, Linda Mshana, ameeleza kuwa lengo la ushiriki wao ni kutoa elimu ya mikopo na kuhamasisha wananchi kuhusu fursa zinazopatikana kupitia mfuko huo, ikiwa ni pamoja na kukopa kwa masharti nafuu.
“Kumekuwa na wahanga wengi sana wa mikopo umiza inayojulikana kama ‘Kausha Damu’, hasa kutokana na kukosa elimu sahihi.
Tunatoa elimu hii ili watu waweze kuuliza maswali muhimu kabla ya kuingia kwenye mikopo, pamoja na kuwafahamisha fursa zinazopatikana kupitia Mfuko wa SELF,” amesema Mshana.
Mshana aliongeza kuwa mfuko huo umeanzisha tawi jipya katika mkoani Rukwa na wilayani Mlele mkoani Katavi , ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwapa fursa ya kukopa kwa masharti nafuu.
“Tumeanzisha aina mpya ya mkopo ambayo itawawezesha wananchi kukopa kwa masharti nafuu zaidi. Moja ya changamoto kubwa ilikuwa kwenye dhamana, lakini sasa tumeshirikiana na wadau ili kuhakikisha dhamana inapunguzwa na wananchi wanapata mikopo kwa dhamana ndogo,” aliongeza.
Aidha, aliwataka wananchi kutembelea banda lao ili kupata elimu zaidi juu ya maswali muhimu ya kuuliza kabla ya kukopa, kama vile kiwango cha riba, muda wa kulipa mkopo, na masharti ya urejeshaji ili kuepuka mikopo yenye madhara kwa biashara zao.
Kwa upande mwingine, Mshana alibainisha kuwa matawi mapya yaliyofunguliwa yamepokelewa vizuri na wananchi, hususan wale wanaojihusisha na kilimo.
“Tumepokea muitikio mzuri, hasa kutoka kwa wajasiriamali na wafanyabiashara. Kwa sasa, tumepata takribani wateja 50 kutoka eneo hilo, licha ya kuwa tawi limefunguliwa kwa kipindi cha miezi miwili pekee,” alihitimisha Mshana.