Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC (SEOM) katika Uchaguzi Mkuu wa Botswana, Mhe. Mizengo Pinda, amezindua misheni hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza la SADC la Siasa, Ulinzi na Usalama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, jijini Gaborone, Botswana.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Pinda aliwasihi wapiga kura wa Botswana kujitokeza kwa kwa wingi kupiga kura tarehe 30 Oktoba 2024, kufanya mamuzi sahihi, kuheshimu mitazamo tofauti ya kisiasa na kuwajibikaji katika kipindi cha baada ya uchaguzi, bila kujali chama au mgombea anayependwa na atakayechaguliwa na wananchi wengi.
“Katika siku zilizobaki kuelekea siku hii muhimu kwenu, SADC inawasihi wote kujitokeza kwa wingi, kufanya maamuzi sahihi, kuheshimu mitazamo tofauti ya kisiasa, na kuwajibika katika kipindi cha baada ya uchaguzi, bila kujali chama au mgombea anayependwa atakayechaguliwa na wananchi,” alisema Mhe. Pinda.
Alisema SEOM inatekeleza jukumu la uangalizi wa uchaguzi katika nchi wanachama, kwa kuzingatia misingi na miongozo ya SADC ya uchaguzi wa Kidemokrasia, ambayo Nchi Wanachama wa SADC waliridhia kutekeleza.
Mhe. Pinda alisema misingi na miongozo hiyo inatoa mbinu za kisayansi na za kimantiki za kuangalia uchaguzi ili kuchangia katika kuimarisha demokrasia katika ukanda huo kwa kuboresha mbinu bora za uchaguzi na kushughulikia kasoro zozote za uchaguzi na kuongeza kuwa misingi na miongozo hiyo pia inategemea nyaraka muhimu za Umoja wa Afrika (AU), kama vile Mkataba wa Afrika wa Demokrasia, Uchaguzi, na Utawala wa mwaka 2007, pamoja na Mikataba husika ya Umoja wa Mataifa (UN).
Alifafanua kuwa kwa kufuata masharti ya misingi na miongozo ya SADC inayohusiana na uchaguzi wa kidemokrasia ya mwaka 2021 na mifumo, kanuni, na taratibu za SEAC, Baraza la Ushauri wa Uchaguzi la SADC (SEAC) lilifanya tathmini ya awali ya uwezo wa uchaguzi nchini Botswana tarehe 22 hadi 29 Aprili 2024.
Alisema lengo la misheni hiyo lilikuwa kutathmini kama mazingira ya kisiasa na usalama nchini Botswana yanaruhusu kufanyika kwa uchaguzi kwa kufuata kanuni na miongozo, mfumo wa kisheria unaoshughulikia uchaguzi uko katika nafasi, mipaka ya majimbo ilitekelezwa kwa mujibu wa sheria ya nchi, na kama Tume Huru ya Uchaguzi (IEC) ya Botswana iko tayari kufanya uchaguzi wa kidemokrasia.
Aliongeza kuwa wakati huo, misheni hiyo ilifanya mazungumzo na wadau kutoka katika sehemu mbalimbali nchini Botswana, ikiwemo vyama vya siasa, mashirika ya kiraia, wataalamu wa uchaguzi, mashirika ya dini, na jumuiya ya kidiplomasia.
Alisema jukumu la SEOM ni kuangalia kama Nchi Wanachama wanafanya uchaguzi kwa kuzingatia Misingi na Miongozo ya SADC iliyorekebishwa mwaka 2021.
“Tupo hapa kusaidiana kuboresha ubora wa chaguzi zetu na ubora wa harakati zetu za muda mrefu kwa ajili ya uhuru na demokrasia.”
Mhe. Pinda alisema SEOM itatoa taarifa yake ya awali kuhusu uchaguzi wa Botswana tarehe Mosi Novemba 2024, na ripoti ya mwisho itawasilishwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Botswana siku 30 baada ya uchaguzi.
Naye Katibu Mtendaji wa SADC, Mhe. Elias Magosi, alisema ndoto ya kubadilisha kanda ya SADC kuwa kanda iliyoungana kikamilifu yenye kuhifadhi ustawi kwa wote inategemea uwezo wake wa kudumisha demokrasia, utawala bora, amani na utulivu na ndoto hiyo itakamilika pale Nchi Wanachama zitakapozingatia na kutekeleza mapendekezo ya SEOM kikamilifu.
“Uzingatiaji wa Misingi na Miongozo ya SADC unatarajiwa kuziinua Nchi Mwanachama wa SADC na utafanya kanda hii kufikia Mpango wa Maendeleo wa Kistratejia wa Kanda (RISDP), Dira ya SADC 2050 na Ajenda pana ya Umoja wa Afrika ya 2063 kuhusu Afrika tunayotaka, bila kuacha Nchi Mwanachama au mtu yeyote nyuma,” alisisitiza.
Alisema SADC inaendelea kuzihimiza Nchi Wanachama kufikiria utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na misheni mbalimbali za uchaguzi (SEOMs) na kuongeza kuwa SEOM hutoa mapendekezo yake baada ya kuzingatia ripoti za waangalizi wake na mitazamo ya wadau mbalimbali wanaoshirikiana nao katika nchi zinazofanya chaguzi.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa mapendekezo ya SEOM utachangia na kukuza demokrasia kwa Nchi Wanachama, kuhakikisha utawala bora na kuimarisha imani ya wananchi na wadau wa nje na kusisitiza kuwa uangalizi wa uchaguzi, ambao una gharama kubwa, unafaida na ni kitu cha thamani, na si kitu tu cha kutimiza wajibu na safari rahisi kwa waangalizi.
Hafla hiyo ya uzinduzi ilihudhuriwa na Baraza la Ushauri wa Uchaguzi la SADC, Wawakilishi wa Serikali ya Botswana, Jumuiya ya wanadiplomasia waliyopo Botswana, Tume Huru ya Uchaguzi ya Botswana (IEC), vyama vya kisiasa, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya Habari na wanahabari, waangalizi wa uchaguzi wa ndani, waangalizi wa kimataifa, vyama vya kiraia na waangalizi wa SADC.
SEOM inajumuisha wajumbe 72, kutoka nchi wanachama wa Troika na SEAC, Wajumbe wa Sekretarieti ya SADC, waangalizi wa SEOM ambao wametoka katika Nchi 10 Wanachama wa SADC za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Falme ya Eswatini, Falme ya Lesotho, Jamhuri ya Malawi, Jamhuri ya Msumbiji, Jamhuri ya Namibia, Jamhuri ya Afrika Kusini, Jamhuri ya Zambia na Jamhuri ya Zimbabwe ambao watakwenda katika wilaya zote, miji, na majiji makubwa ya Jamhuri ya Botswana.