Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imetoa fursa maalum wiki hii ya kutoa mafunzo kuhusu masuala ya fedha, ikiwemo nafasi ya kueleza majukumu yake kwa wanafunzi wa vyuo vya VETA na Chuo cha IFM mkoani Mbeya . Lengo kuu ni kuwafanya wanafunzi hao kuwa mabalozi wa kuelimisha wenzao kuhusu masuala ya bima na benki.
Akizungumza katika Viwanja vya Luanda Nzovwe Mbeya kwenye wiki ya huduma za kifedha Bertha Hyera, afisa wa bodi hiyo amesema, walikuwa na madarasa mawili: darasa la kwanza lilihusisha wanafunzi kutoka vyuo vya VETA, na darasa la pili lilihusisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza kutoka Chuo cha IFM.
“Hayo makundi yote mawili ni muhimu kwa masuala ya fedha, hasa benki, kwani wanafunzi hawa ndio kwanza wanafungua akaunti za benki. Tuliona ni vyema kuwaelimisha kuhusu Bodi ya Bima ya Amana kwa sababu hawa ni wateja wapya kabisa, na ni wadau ambao wanahitaji kufahamu vizuri kuhusu bima,” alisema Iyela.
Alieleza kuwa changamoto kubwa waliyokutana nayo ni kwamba elimu kuhusu masuala ya kibenki ilikuwa ni mpya kwa wanafunzi hao. “Tulijitahidi kuwaelimisha kuhusu jinsi ya kusoma taarifa za benki ili kujua ni benki gani inatengeneza faida na zipi hazipo katika hali nzuri kifedha. Hii ni muhimu ili kupunguza hatari ya kuweka fedha kwenye benki zisizo imara.”
Hyera aliongeza kuwa elimu hii itawasaidia wanafunzi kuingia kwenye benki zenye nguvu kifedha na kutowahofia benki zinapofilisika au kufungwa. Pia aliwashauri wanafunzi kuwafahamisha ndugu, jamaa na marafiki kuhusu umuhimu wa elimu hii.
Kwa upande wake Thuwaiba Juma, Afisa wa Bodi ya Bima ya Amana amesema DIB inasimamia amana za fedha zinazohifadhiwa kwenye mabenki yaliyopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania. Lengo kuu la taasisi hiyo ni kusimamia mfuko wa Bima ya Amana, ambao huchangiwa na mabenki yote yenye leseni mara moja kwa mwaka kwa asilimia 0.15 ya wastani wa amana wanazopokea kwa mwaka mzima.
Aliongeza kuwa jukumu lingine la bodi ni kulipa fidia kwa wateja wa Benki ambao watakuwa na amana kwenye benki zinazopata matatizo ya kifedha.
“Pindi benki inapofutiwa leseni, Bodi ya Bima ya Amana italipa fidia kwa wateja waliokuwa na amana kwenye benki husika.
Fidia hii inalipwa kuanzia shilingi 1 mpaka shilingi milioni 7.5 kwa mujibu wa sheria.
Kwa wateja wenye mikopo watakuwa na utaratibu maalum wa kurudisha mikopo yao, na wateja ambao wanastahili watalipwa fidia kulingana na sheria husika baada ya Mali za Benki iliyofilisika kupigwa mnada.