Matukio mbalimbali ya mashindano ya kuogelea ya HPT Mixed and Open yaliyofanyika kwenye Bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) Masaki.
………………
*Waogeleaji saba wavunja rekodi yashindano ya HPT 2025
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Jumla ya waogeleaji saba walivunja rekodi katika Mashindano ya High Performance Training (HPT) Mixed na Open Swimming, yaliyomalizika mwishoni mwa wiki katika bwawa la kuogelea la International School of Tanganyika (IST) Masaki, jijini.
Mashindano hayo yalishirikisha zaidi ya waogeleaji 150, yaliandaliwa kwa lengo la kuwapima uwezi waogeleaji kwa ajili ya mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Katika mashindano hayo, waogeleaji wawili waling’ara zaidi kwa kuvunja rekodi mbili za HPT kila mmoja na kuzawadiwa Sh1 milioni kutoka kwa waandaaji katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Pepsi, International School of Tanganyika (IST), JD Events, na City Ambulance.
Nicolene Viljoen (12) wa klabu ya Riptides alivunja rekodi ya mita 200 Individual Medley, akitumia muda wa 2.34.90 na kuvunja rekodi ya awali ya 2.44.76.
Nicolene pia alivunja rekodi ya mita 100 Breaststroke, akimaliza kwa muda wa 1.21.33 na kufuta rekodi ya awali ya 1.25.83.
Pia Phares Mteki (8) wa klabu ya Ziwa Victoria alivunja rekodi mbili. Phares aliweka rekodi mpya katika mita 50 freestyle kwa muda wa 34.11, akipiku rekodi ya awali ya 35.42.
Pia alivunja rekodi ya mita 50 butterfly, akimaliza kwa 39.52 na kuvunja rekodi ya awali ya 43.71.
Waogeleaji ambao walizawadiwa Sh500,000 kwa kuvunja rekodi moja ni pamoja na Heydleen Kagashi (11) kutoka Taliss-IST swimming Club, aliyeboresha rekodi ya mita 100 freestyle kwa muda wa 1.09.13, akipiku rekodi ya awali ya 1.21.33.
Pia Aryiel Angemi (12) kutoka Taliss-IST alivunja rekodi ya mita 50 freestyle, akitimka kwa 28.31 na kuvunja rekodi ya awali ya 38.38.
Muogeleaji wa Dar es Salaam Swimming Club (DSC), Konhelli Mhella (9), aliweka rekodi mpya ya mita 50 freestyle kwa muda wa 32.89, akipiku rekodi ya awali ya 32.90.
Mwingine kutoka Dar Swim Club, Austin Okore (15), aliweka muda mpya wa 31.45 na kuvunja rekodi ya awali ya 31.98.
Pia Mina Siebert (10) kutoka HPT aliweka muda mpya wa 24.63 katika mita 100 butterfly, akipiku rekodi ya awali ya 28.71.
Meneja wa HPT, Francisca Binamungu, aliwapongeza waogeleaji wote, makocha, viongozi, na wadau kwa mafanikio ya mashindano hayo.
“Tumefikia lengo letu kwani waogeleaji wengi wametengeneza muda mpya wa kuogelea (PBs) huku wengine wakivunja rekodi.
Hii ni hatua kubwa kwa mchezo huu, na lengo letu ni kuona waogeleaji wakiboresha uwezo wao kila siku ili kushindana si tu hapa nchini bali pia kimataifa kwa kufikia viwango vya kufuzu,| alisema Francisca.
Kocha wa timu ya taifa ya kuogelea ya Tanzania, Alexander Mwaipasi, alionyesha kuridhishwa na maendeleo ya waogeleaji hao, akisema, “Nimevutiwa na viwango vilivyoonyeshwa na waogeleaji. Tuko kwenye mwelekeo mzuri, na naamini watafanikiwa katika mashindano ya kimataifa yajayo. Hili ndilo lengo kuu la HPT.”
Kocha mwingine, Michael Livingstone, alisema kuwa waogeleaji wa Tanzania wanaweza kufikia viwango vya kufuzu kwa World Aquatics B.
Matokeo ya timu kwa jumla kwa wanawake na wanaume
Klabu ya Taliss-IST iliongoza kwa alama 1,309, ikifuatiwa na Dar es Salaam Swimming Club yenye alama 1,232 na Bluefins Swimming Club kwa alama 239.
Pia klabu ya High Performance Training ilikusanya alama 128, huku FK Blue Marlins wakipata alama 51.
Matokeo ya jumla kwa upande wa wanawake
Taliss-IST ilimaliza nafasi ya kwanza kwa alama 722, ikifuatiwa na Dar es Salaam Swimming Club yenye alama 559 na Bluefins Swimming Club yenye alama 170.
High Performance Training ilikusanya alama 94, Riptides alama 57, na FK Blue Marlins wakipata alama 15.
Matokeo ya jumla kwa upande wa wanaume
Timu ya wanaume Dar es Salaam Swimming Club iliongoza kwa alama 673, ikifuatiwa na Taliss-IST yenye alama 587 na Bluefins Swimming Club yenye alama 69.
Klabu ya FK Blue Marlins ilikusanya alama 36, High Performance Training ilipata alama 34, na Klabu ya Michezo ya Ziwa Victoria ilimaliza kwa alama 30.