Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kampasi ya Tabora katika kikao kilichofanyika chuoni hapo mkoani Tabora.
Kaimu Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) akiwasilisha ripoti ya chuo wakati wa kikao kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya UtumishiwaUmma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (kulia) na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kampasi ya Tabora
Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma kampasi ya Tabora, Dkt. Ramadhan Marijani akijibu hoja za Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (kushoto) wakati wa kikao kati ya Naibu Waziri na watumishi wa chuo hicho.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akichapa kwa mashine alipotembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kampasi ya Tabora. Wanaoshuhudia ni Kaimu Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Emmanuel Shindika (kushoto) na Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma kampasi ya Tabora, Dkt. Ramadhan Marijani
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akikagua jengo jipya la ghorofa mbili la Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kampasi ya Tabora. Wengine ni Mkurugenzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma tawi la Tabora, Dkt. Ramadhan Marijani na watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.
***********************************************
Serikali imepanga kushindanisha huduma zinazotolewa na kampasi za
Chuo cha Utumishi wa Umma nchini ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi
kwa watumishi wa chuo hicho, lengo likiwa ni kuboresha huduma
zinazotolewa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa
ziarayake ya kikazi mkoani Tabora ya kutembelea Chuo cha Utumishi wa
Umma, kampasi ya Tabora ili kukagua utekelezaji wa miradi na kuhimiza
uwajibikaji kwa watumishi wa chuo hicho.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, kampasi zitakazoshindanishwa ni za Dar
es Salaam, Mtwara, Tabora, Singida, Tanga na Mbeya ambapo ameweka
bayana kuwa, kampasi itakayoshinda katika utoaji wa huduma bora
itapewa tuzo.
“Utawekwa utaratibu ambao utashindanisha kampasi zote kwa kuzingatia
vigezo stahiki ili kumpata mshindi anayestahili" Mhe. Dkt. Mwanjelwa
amesisitiza.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amefafanua kuwa, mashindano hayo yatakuwa ni
chachu ya kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa kila mtumishi na
kuongeza kuwa ufanisi huo utakiletea sifa chuo kuwa taasisi mahiri
inayotoa mafunzo ya uhazili, menejimenti ya ofisi, utunzaji kumbukumbu na
nyaraka za kiutumishi.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa kampasi zote za
chuo hicho kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kutimiza malengo ya chuo.
Akizungumzia kuhusu uendeshaji wa kampasi ya Tabora, Mhe. Dkt.
Mwanjelwa ameiagiza menejimenti ya chuo hicho kuhakikisha kampasi
hiyo inajiendesha kwa mapato ya ndani badala ya kutegemea ruzuku
kutoka serikali kuu.
“Lazima muwe na vyanzo mbadala vya mapato ya ndani vitakavyosaidia
uendeshaji wa ofisi. Mapato hayo yatoke kwenye vyanzo halali
vinavyozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo” Mhe. Dkt. Mwanjelwa
ameongeza.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amehitimisha ziara yake ya kikazi kwa kutembelea
majengo ya chuo hicho katika kampasi ya Tabora na kujionea maabara ya
kompyuta, maabara za mashine za kuchapa, maktaba,mabweni ya
wanafunzi na jengo jipya la ghorofa mbili linalotarajiwa kutumika kwa
matumizi ya maktaba, chumba cha kompyuta, ofisi, madarasa na kumbi za
mikutano.