Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na wanariadha pamoja na wananchi waliojitokeza katika Mashindano ya John Stephen Akhwari International Marathon yaliyofanyika Juni 09 Jijini Arusha yaliyokuwa na lengo la kumuenzi Mwanariadha John Stephen Akhwari ambaye ameletea heshima Taifa mwaka 1968 aliposhiriki mbio za Km 42 nchini Mexico. Kushoto ni Rais wa Shirikisho la Riadha nchini ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Antony Mtaka na Kulia ni Mwanariadha huyo Mzee John Stephen Akhwari.
Na Shamimu Nyaki -WHUSM
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ameiagiza Idara ya Michezo ya Wizara hiyo kushirikiana na Waandaaji wa Mashindano ya John Stephen Akhwari International Marathon kufanya mashindano hayo kila mwaka ili kumuenzi Mwanariadha huyo aliyeliletea Taifa heshima kubwa.
Mhe. Mwakyembe ametoa agizo hilo jana Jijini Arusha wakati alipofungua mashindano hayo yaliyofanyika kwa lengo la kutambua na kuenzi mchango wa Mwanariadha huyo ambaye aliitangaza nchi kupitia mchezo huo mwaka 1968 huko nchini Mexico wakati aliposhiriki mbio za Km 42 ambapo licha ya kuumia goti wakati wa mbio alikataa kusitisha mbio hizo na kuendelea kukimbia hadi alipomaliza kitendo kilichoonekana kuwa ni cha kizalendo kwa nchi yake.
“Serikali inatambua mchango mkubwa uliofanywa na Mwanariadha huyu John Stephen Akhwari katika mchezo wa riadha ndio maana nimeiagiza Idara ya Michezo kuhakikisha kuwa mashindano haya yanafanyika kila mwaka ili kuenzi uzalendo wa Mzee Akhwari”, Alisema Dkt. Mwakyembe.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akimkabidhi Mzee John Stephen Akhwari tuzo ya heshima kutokana na mchango wake mkubwa katika mchezo wa riadha hapa nchini mara baada ya kumalizika kwa Mashindano ya John Stephen Akhwari International Marathon yaliyofanyika Juni 09 Jijini Arusha yaliyokuwa na lengo la kumuenzi Mwanariadha huyo ambaye ameletea heshima Taifa mwaka 1968 aliposhiriki mbio za Km 42 nchini Mexico. Wanaoshuhudia ni viongozi wa Shirikisho la Riadha hapa nchini.
Aidha Mhe. Mwakyembe amewataka wachezaji wote nchini kucheza na kushiriki mashindano mbalimbali kwa lengo la kufaidika katika maisha yao kwa kuwa michezo katika ulimwengu wa sasa ni ajira hivyo lazima waongeze juhudi zaidi ili waweze kujitangaza ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Riadha nchini Mhe. Antony Mtaka amesema kuwa Mkoa wa Simiyu ambao ndiye anaoungoza kama Mkuu wa Mkoa tayari umeanza kujenga shule maalum ya michezo ili kufundisha vijana wengi zaidi ambao watakuwa na uwezo pamoja na vipaji vizuri katika michezo.
Vile vile Mhe. Mtaka amesema kuwa mchezo wa Riadha umeendelea kufanya vizuri hapa nchini kutokana na vijana wengi kujitokeza kucheza mchezo huo na kuahidi kuwa Shirikisho la Riadha nchini lipo tayari kufundisha wanariadha ambao wapo tayari kujifunza.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akipokea cheti cha utambuzi wa mchango wake katika mchezo wa riadha kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Riadha nchini ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Antony Mtaka(kushoto) mara baada ya kumalizika kwa Mashindano ya John Stephen Akhwari International Marathon yaliyofanyika Juni 09 Jijini Arusha yaliyokuwa na lengo la kumuenzi Mwanariadha huyo ambaye ameletea heshima Taifa mwaka 1968 aliposhiriki mbio za Km 42 nchini Mexico. Kushoto ni Mzee John Stephen Akhwari.
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akimvalisha Medali mshindi wa kwanza wa mbio za Km 21 kwa wanaume Bw. Emmanuel Giniki katika mashindano ya John Stephen Akhwari International Marathon yaliyofanyika Juni 09 Jijini Arusha yaliyokuwa na lengo la kumuenzi Mwanariadha huyo ambaye ameliletea heshima Taifa mwaka 1968 aliposhiriki mbio za Km 42 nchini Mexico.