Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa kushirikiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, zimesaini hati 11 za makubaliano ya kibiashara, ambapo sita ni baina ya serikali na mitano ni ya sekta binafsi. Lengo la makubaliano hayo ni kukuza diplomasia na uchumi kati ya nchi hizi mbili.
Akizungumza leo, Oktoba 19, 2024, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa tano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC), alieleza kuwa ushirikiano huo ni fursa kubwa kwa Tanzania, kwani utachochea ukuaji wa uchumi na kuboresha sekta mbalimbali nchini.
Balozi Kombo alisema kufikiwa kwa makubaliano hayo ni matokeo ya juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha nchi inapiga hatua na uchumi unakua. Aliwasihi Watanzania, hususan wale wanaojihusisha na biashara kama Chemba ya Biashara na TanTrade, kuchangamkia fursa hizi ili kuimarisha uchumi wa taifa.
“Namshukuru sana Rais wa Tanzania na Rais wa Iran kwa kuimarisha ushirikiano huu wa pande mbili. Ushirikiano huu utachochea maendeleo katika sekta za biashara, uwekezaji, kilimo, nishati, ulinzi, usalama, na elimu,” alisema Balozi Kombo.
Aidha, aliongeza kuwa Tanzania na Iran pia zitashirikiana katika sekta za afya, sayansi na teknolojia, pamoja na utamaduni.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Golamreza Nouri Ghezelcheh, alieleza kuwa ushirikiano huu katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, utasaidia nchi zote mbili kuboresha shughuli zao za kilimo kwa maslahi ya wananchi.
“Marais wa pande zote mbili wamehimiza uendelezaji wa uhusiano kati ya Afrika na Iran, na nina matumaini kuwa makubaliano haya yataleta uhusiano mzuri zaidi katika awamu hii mpya,” alisema Nouri Ghezelcheh.
Hafla ya kusaini makubaliano hayo imefanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ambapo ilihusisha wizara za kisekta, baadhi ya taasisi za umma, na taasisi binafsi.