NA VICTOR MASANGU,KIBAHA
Mganga mkuu wa Halmashauri ya Kibaha mji Dkt.Cathirine Saguti amesema kwa uwepo wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii unachangia kwa kiasi kikubwa kuibua wagonjwa wapya kwa watoto na Wanawake ambao wanakuwa wanafanyiwa ukatili kwenye maeneo yao.
Dkt.Catherine amesena wahudumu hao katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha wamefanikiwa kuibua wagonjwa 113 kati ya 242 ambao ni zaidi ya asilimia 45 ya waliokuwa na maambukizi ya Kifua kikuu katika kipindi cha 2023/2024.
Mganga mkuu wa Halmashauri hiyo Dk.Catherine Saguti aliyabainisha hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa yake ya kazi zinazofanywa na kundi hilo wakati wakipokea baiskeli kutoka Shirika la Buffalo Bicycle kwa ajili ya kuwarahisishia usafiri wahudumu hao.
Dk Saguti alisema wahudumu hao pia wameibua watoto 4,797 waliokuwa wanaishi katika mazingira hatarishi sambamba na Wanawake 87 na watoto 127 waliofanyiwa ukatili wa kijinsia.
Alisema mbali ya mafanikio hayo yaliyotokana na kazi za wahudumu wa afya ngazi ya jamii katika Halmashauri hiyo wamekuwa wakihamasisha wananchi kupata chanjo na kushirikiana na Jamii kutoa elimu ya lishe.
Afisa Mipango wa Taifa Huduma za afya ngazi ya jamii Bahati Mwailafu alisema Mpango Jumuishi wa huduma za jamii unaotekelezwa katika mikoa yote 26 na kwamba kwasasa wameanza na mikoa 10 ya kipaumbele ikiwemo Pwani, Lindi, Mbeya na Kagera.
Alisema katika mikoa hili Halmashauri mbili ndizo zitakazoqnza utekelezaji wa Mpango na kwa Mkoa wa Pwani ni Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji na Mji wa Kibaha .
Aliiwashukuru wadau hao kwa kusaidia usafiri unaokwenda kuwarahisishia wahudumu hao kufikia Jamii kwa urahisi huku akiomba wadau wengine kujitokeza kusaidia kundi hilo
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa alisema uwepo wa vituo vingi vya kutolea huduma za afya kumesababisha kuwa na uhitaji wa watoa huduma wengi zaidi na hivyo kupatikana kwa baiskeli hizo zinakwenda kusaidia kuwafikia wananchi walip wengi
Alisema Serikali inaendelea kuboresha vituo vya kutolea huduma za afya na kwamba katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha imefaikiwa kujenga kituo cha afya Kongowe kuwapunguzia wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Akipokea baiskeli hizo Mwenyekiti wa huduma za Jamii wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni Diwani wa Visiga Kambi Legeza alisema upatikanaji wa usafiri huo utaongeza utendaji kazi kwa wahudumu hao wa huduma za afya ya Jamii.
Buffalo Bicycle walibainisha kwamba mbali ya kutoa baiskeli hizo 146 katika Halmashauri ya Mji Kibaha malengo yao ni kutoa baiskeli 10,000 hapa nchini kulingana na uhitaji.