Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimefanikiwa kupata miradi 11 yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 4.5 kati ya mwezi Mei na Oktoba 2024.
Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Raphael Chibunda, alieleza mafanikio hayo wakati wa mahafali ya 44 ya chuo yaliyofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe, Morogoro. Mahafali hayo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali, wakiwemo wakuu wa vyuo na Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania.
Profesa Chibunda alibainisha kuwa SUA imeendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo katika kutekeleza mpango wa BBT (Building Better Tomorrow), unaolenga kutafuta fursa za ajira za muda na endelevu kwa vijana.
“SUA imepewa jukumu la kusaili na kujaza nafasi 2,000 za wagani wa zao la pamba. Kufikia sasa, baada ya usaili wa awamu ya tatu, tumepata wagani 700, na usaili wa awamu ya nne utaendelea hivi karibuni,” alisema Profesa Chibunda.
Aliongeza kuwa kupitia mpango huu, wahitimu wa Shahada ya Kilimo na Vipando wamekuwa na uhakika wa kupata ajira, na baadhi ya wahitimu wa leo tayari wamefanya usaili na kufaulu.
Katika mwaka wa masomo 2024-2025, SUA imedahili jumla ya wanafunzi wapya 5,663 waliojisajili na kuthibitishwa kujiunga na chuo hicho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la SUA, Mhe. Jaji Chande Othman, alieleza kuwa baraza limeidhinisha mapitio ya Mpango wa Miaka 10, kuanzia mwaka 2024 hadi 2034.
“Ili kuboresha mafunzo na kuongeza ujuzi kwa wahitimu, Baraza la Chuo limehimiza umuhimu wa mafunzo kwa vitendo kwa kuboresha mashamba darasa, karakana za uhandisi, na maabara za mafunzo ya misitu, ili kuwapa wanafunzi na wadau fursa ya kuongeza maarifa kupitia vitendo,” alisema Jaji Othman.
Mahafali ya 44 ya SUA yamehusisha jumla ya wahitimu 3,061, wakiwemo wanaume 1,650 na wanawake 1,411, sawa na asilimia 46.1 ya wahitimu.