Na Sophia Kingimali.
WAZIRI wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Shamata Khamis amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, imeweka mikakati mbalimbali katika kuhakikisha Tasnia ya kuku na ndege wafugwao inakua na kuchangia zaidi katika ajira na kukuza uchumi lakini pia kuimarisha usalama wa chakula na lishe.
Hayo ameyasema leo Octoba 17,2024Jijini Dar es salaam mara baada ya kufunga jukwaa la Tasnia ya kuku na ndege ambapo amesema Mikakati hiyo ni pamoja na Kuanzisha mashamba ya kuku na ndege wafugwao.
“Serikali itafanya Uwekezaji katika maeneo ya kutotoleshea vifaranga vya kuku,
Kuanzishwa kwa kiwanda kipya cha vyakula vya mifugo,
Kuanzishwa kwa machinjio mapya ya kuku, ambayo
Yatawekeza katika maabara ya mifugo na uwezo wa uchunguzi, pamoja na uzalishaji wa chanjo za mifugo na Kuanzisha vituo vya utafiti wa kuku”,amesema.
Aidha ameongeza kuwa,Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetekeleza afua mbalimbali katika kuhakikisha Tasnia ya kuku inakua na kuleta tija
“Afua ambazo SMZ inatekeleza ni pamoja na kuwajenga uwezo wa wataalamu wa mifugo wa ndani katika mbinu za kisasa za ufugaji bora na udhibiti wa magonjwa, kujenga uwezo wa wafugaji kwa kutoa mafunzo, mbinu na kanuni za ufugaji bora wa kuku na ndege wafugwao ili kuongeza tija ya uzalishaji, kuweka mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa ya kuku na ndege wafugwao ili kudhibiti milipuko ya magonjwa pamoja na kuimarisha utekelezaji wa afua za Afya moja kwa moja ” Amesema Waziri Khamis.
Katika hatua nyingine waziri khamis amesema kuwa mikakati ambayo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatekeleza, ni pamoja na kushirikana na wadau wa maendeleo sekta binafsi na wawekezaji ili kuleta mageuzi ya haraka kwenye Tasnia ya kuku na ndege .
Ameongeza kuwa wataendelea Kufungamanisha kanuni na viwango vya ufugaji kuku katika nchi za SADC ili kuwezesha biashara za kikanda na kuhakikisha usalama wa mazao ya kuku na bidhaa zake
Amesema wataendeleza programu za mafunzo za kikanda kwa wafugaji, madaktari wa mifugo na wafanyakazi wa ugani ili kuongeza ujuzi katika usimamizi wa kisasa wa kuku na ustawi wa wanyama.
Amesema wataendelea kufanya uwekezaji katika Miundombinu ya uzalishaji wa kuku na ndege wafugwao,ambapo miundombinu hiyo ni kama vile vyumba baridi (cold room facilities), machinjio na vifaa vya usindikaji .
Aidha ametoa rai kwa Jumuiya za Kikanda na Kimataifa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha tasnia ya kuku na ndege wafugwao, ili kupunguza na kuondoa changamoto na vikwazo vilivyopo katika tasnia hiyo.
Naye Mshiriki wa mkutano huo Fatuma rashidi amesema kuwa mkutano huo umekuwa na manufaa makubwa kwani wameweza kujifunza mambo mbalimbali kuhusu tasnia ya kuku na ndege na uzalishaji kwa ujumla hivyo wataenda kubadilisha namna ya ufugaji wao na kufuga kwa tija ili wajipatie kipato.