Na Ashrack Miraji – Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni, amesema kuwa zoezi la uandikishaji wananchi kwenye Daftari la Mkazi linaendelea kwa mafanikio, huku wananchi wengi wakiwa wamehamasika na tayari wameshajiandikisha kwenye vituo mbalimbali.
DC Kasilda alitoa kauli hiyo Oktoba 11, 2024, baada ya kujiandikisha mwenyewe katika Daftari la Mkazi kwenye Kituo cha Stesheni, kilichopo katika Kata ya Stesheni. Kituo hiki ni mojawapo ya vituo 503 vya uandikishaji vilivyopo Wilayani Same.
Aidha, DC Kasilda aliwasisitiza wakazi wa Same kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vilivyoko katika maeneo yao ili kujiandikisha, hatua ambayo itawapa uhalali wa kushiriki katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
“Nimeshajiandikisha rasmi kama Mkuu wa Wilaya, na pia nimepata fursa ya kukagua baadhi ya vituo ili kuona maendeleo ya zoezi hili. Nimefarijika kuona wananchi wamehamasika na uandikishaji unaendelea vizuri,” alisema DC Kasilda.
Zoezi hili la uandikishaji kwenye Daftari la Mkazi lilianza rasmi Oktoba 11, 2024, na litadumu hadi Oktoba 20, 2024, likiwa na kauli mbiu isemayo, “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi.”