Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Septemba 9, 2024
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (Mb), amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, pamoja na Wakala wa Majengo ya Watumishi wa Umma (TBA) kufanya uchambuzi wa mfumo katika kujenga nyumba za watumishi kwa gharama nafuu.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba nane za wakuu wa idara wa Halmashauri ya Chalinze, mkoani Pwani, zilizogharimu sh. milioni 960.5, Bashungwa alielekeza TBA kuwa wabunifu katika kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba za watumishi.
“Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na TBA wafike hapa Chalinze kujionea na kujifunza kuhusu nyumba hizi za kisasa ili kupata mbinu bora za kuboresha na kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba kwa watumishi wa halmashauri, miji, na majiji mengine,” alisema Bashungwa.
Aidha, Waziri Bashungwa aliwataka watumishi kuwa wazalendo na kuacha urasimu wanapotoa huduma kwa wananchi. Pia alisema nyumba hizo zinapaswa kuwa chachu na motisha kwa watumishi hao kufanya kazi kwa bidii.
“Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kuboresha mazingira ya watumishi. Nakupongeza Mkurugenzi wa Halmashauri, Ramadhani Possi, watendaji, na Mbunge Ridhiwani Kikwete kwa utekelezaji wa ilani, Kwa hakika mmejipanga kimkakati na kazi inaonekana,” aliongeza Bashungwa.
Katika ziara hiyo, Waziri Bashungwa pia alizindua soko jipya la Chalinze lililogharimu sh. bilioni 1.7 na kuwashauri wajasiriamali kuwa wabunifu katika kuanzisha biashara tofauti ili waweze kupata soko kirahisi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Miundombinu cha Halmashauri ya Chalinze, Injinia Olais Sikoi, ujenzi wa nyumba nane za wakuu wa idara ulianza mwaka 2022 na kufikia asilimia 98 kukamilika.
Sikoi aliongeza kuwa, nyumba hizo zimeisaidia halmashauri kuokoa fedha ambazo hapo awali zilitumika kuwalipia wakuu wa idara pango la nyumba, na badala yake, fedha hizo sasa zinaweza kuelekezwa kwenye shughuli za maendeleo.