Na Sophia Kingimali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu Sera,Bunge na Wiliam Lukuvi amevisihi vyama vya siasa nchini kuacha kuwa na siasa za mihemko na badala yake wafanye siasa zenye hoja na maelewano.
Pia amevipongeza vyama vya siasa nchini kwa kuendelea kulinda umoja na amani ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere kwani umoja na amani utaendelea kuimarika ikiwa kila chama cha siasa kitafuata salsafa ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kutaka maridhiano,ustahimilivu,mabadiliko na kujenga upya.
Hayo ameyasema leo Octoba 8,2024 ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya kutembelea vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.
“Wanasiasa ndio kila kitu kwa wananchi hivyo endeleeni kutunza amani hii Ili Tanzania iendelee kusonga mbele kwa kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli kwani umoja na amani ndio unaosababisha viongozi wa Serikali kutembelea vyama vya siasa na kufanya mambo mengi ya kimaendeleo ndani ya nchi.”amesema Lukuvi
Akizungumzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu Lukuvi amesema Rais Dk.Samia amehagiza chaguzi hizo zitakazofanyika ziwe za uhuru,heshima na haki kwa faida ya watanzania wote.
“Nawahakikishieni uchaguzi wa mwaka huu utaenda vizuri kwa kufuata Sheria na kanuni zilizowekwa”, amesema.
Aidha Lukuvi ameongeza kuwa Serikali imejipanga kwa kila atakayechaguliwa na wananchi na kupata kura nyingi huyo ndiye atakaye tangazwa mshindi kwa wananchi.
” Kwenye mashindano yeyote ni lazima kuwepo na ushindani hivyo hata uchaguzi wa mwaka huu na mwaka ujao lazima mshindi atapatikana bila ya kujua atatoka chama gani,” amesema.
“Rais Dk.Samia ameniagiza chaguzi za mwaka huu ziwe na mfano kwa sababu anazitaka ziwe na utulivu na ustahimilivu”,amesema.
Nao wanasiasa Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kutembelewa na Waziri Lukuvi viongozi hao wameihakikishia Serikali kuwa kutakuwa na uchaguzi wa utulivu kwa lengo la kulinda amani ya nchi.
“Chama chetu Cha UDP sera yetu kubwa ni upendo na tunajua kuwa siasa si uadui na tutahakikiaha salsafa za Rais Dk.Samia zinatuongoza vyema ,”amesema Cheyo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa chama cha NCCR_MAGEUZI Joseph Selasini amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha chaguzi za mwaka huu zinaenda vizuri huku wakiwahamasisha wanachama wao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katikà daftari la wapiga kura litakaloanza Novemba 11mwaka huu.
Mwenyekiti wa chama Cha wananchi Cuf Ibrahimu Lipumba amesema ameishukuru Serikali kwa kuleta salsafa ya R4 ambayo ndani yake kuna maridhiano.
Nae,Katibu Mkuu wa chama cha NLD Doya Hassan amempongeza Waziri Lukuvi kwa kutenga muda wake na kutembelea vyama vyao kwani hiyo imeonesha kwa vitendo dhamira ya Rais Samia katika kuviunganisha vyama na Serikali hivyo wameahidi kushirikiana vyema pia kuhamasisha wanachama wao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili waweze kushiriki vyema kwenye chaguzi zijazo.
“Naona R4 zimeshaanza kufanya kazi yake hadi leo hii Waziri anatembelea vyama vya siasa ofisini kwao hayo ni mabadiliko makubwa ndani ya sekta ya siasa,”amesema.
Waziri Lukuvi ameanza ziara yake ya kutembelewa vyama vyWAZIRI a siasa 19 vilivyokuwa na usajili wa kudumu Octoba 7 ambapo leo Octoba 8,2024 ametembelea vyama vinne ambavyo ni chama cha CUF,UDP,NCCR-MAGEUZi na NLD.