Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella, ameweka wazi kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina dhamira thabiti ya kuwasaidia wachimbaji wadogo, wakati na wakubwa wa madini, ili kuhakikisha kuwa matunda ya uchimbaji wa dhahabu yanawanufaisha Watanzania wote, hususan katika Mkoa wa Geita.
Shigella alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo, akizungumzia maandalizi ya maonesho ya saba ya Teknolojia katika sekta ya madini, yatakayofunguliwa kuanzia Oktoba 5, 2024 katika viwanja vya EPZ, Bombambili, mkoani Geita. Amesisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa uchumi wa taifa unapata faida zaidi kutokana na dhahabu, badala ya kutegemea fedha za kigeni.
Akizungumzia Sheria mpya ya Madini iliyotungwa na Bunge hivi karibuni, Shigella alisema, “Sheria hii inaelekeza kuwa asilimia 20 ya uzalishaji wa dhahabu ununuliwe na Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Hii inatoa nafasi kwa taifa kuwa na hifadhi ya dhahabu, ambayo ina thamani kubwa zaidi kuliko kuhifadhi fedha za kigeni.”
Alitolea mfano wa ongezeko la thamani ya dhahabu ambapo alisema, “Mwaka jana, kilo moja ya dhahabu ilikuwa ikiuzwa kwa dola elfu 50, lakini sasa imepanda hadi dola elfu 70. Kama tungekuwa tunahifadhi dhahabu yetu, thamani yake ingekuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na fedha za kigeni.”
Shigella aliwataka wafanyabiashara wa dhahabu kuelewa Sheria hii mpya, akibainisha kuwa BoT imetoa utaratibu wa ununuzi wa dhahabu kwa bei nzuri na punguzo kubwa la kodi na tozo. “Bei inayotolewa na Benki Kuu ni nzuri zaidi kuliko maeneo mengine ambayo wachimbaji na wafanyabiashara walikuwa wakiuza dhahabu yao,” aliongeza.
Kwa sasa, mazungumzo yanaendelea kati ya Wizara ya Madini, Tume ya Madini, na baadhi ya wafanyabiashara wa dhahabu walioitwa Dodoma, huku wengine wakiendelea na biashara baada ya kupewa mwongozo na Benki Kuu.
Shigella aliwataka wachimbaji wadogo, wa kati, na wakubwa kuendelea kufanya biashara na Benki Kuu kutokana na urahisi wa utaratibu huo, ambao umetoa nafuu kubwa ikilinganishwa na masoko mengine.
Mnamo Oktoba 1, 2024, BoT ilitoa taarifa kuhusu mpango wa ununuzi wa dhahabu, ikitoa fursa kwa wauzaji kuuza dhahabu zao moja kwa moja kwa Benki Kuu kwa bei ya ushindani wa soko la kimataifa. Mpango huu pia unatoa punguzo la ada na uhakika wa malipo ya haraka kwa wauzaji watakaouza asilimia 20 ya dhahabu zao kwa Benki Kuu, kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Madini Sura ya 123.