Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), kimefanya mafunzo kwa watumishi wa chama na jumuiya zake kuhusu umuhimu wa kujiendeleza kielimu kupitia fursa zinazopatikana kimataifa.
Mafunzo hayo yamefanyika Oktoba 3, 2024 katika ukumbi wa ofisi za Makao Makuu ya CCM, Dodoma na kuhudhuriwa na watumishi wa CCM, Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Jumuiya ya Wazazi (WAZAZI) na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).
Akifungua mafunzo hayo ya siku moja, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Ndg. John Mongella amewataka watumishi wa CCM kuchangamkia fursa za kujiendeleza kielimu ili kuwa weledi katika nafasi wanazozitumikia ndani ya chama na jumuiya zake.
Amesema chama kupitia idara ya SUKI, kitajitahidi kutafuta fursa hizo, lakini mtumishi mmoja mmoja hana budi kuzitafuta kwa njia mbalimbali ikiwemo kutumia mitandao ya kijamii.
Naibu Katibu Mkuu, Ndg. Mongella alifuatana na Katibu wa NEC, ambaye ni Mkuu wa Idara ya SUKI, Ndg. Rabia Abdalla Hamid na Katibu wa NEC, Organaizesheni, Ndg. Issa Gavu.
Kwa upande wake, Ndg. Rabia amesema kujiendeleza kielimu ni muhimu kwa kuwa kunamfanya mtumishi kujipatia maarifa mapya kulingana na mabadiliko mbalimbali yakiwemo ya sayansi na tekinolojia.
Ndg. Rabia alizishukuru nchi ambazo zimekuwa zikitoa fursa za mafunzo kwa watumishi na makada wa CCM, ikiwemo Uingereza ambayo kupitia Taasisi ya Chevening imekuwa ikitoa ufadhili wa masomo kwa Watanzania.
Ndg. Rabia amewapongeza watumishi wa CCM, UWT, WAZAZI na UVCCM kwa kuhudhuria mafunzo hayo, ambayo yamewaongezea mwanga kuhusiana na ufadhili wa masomo unaotolewa na Taasisi ya Chevening kwa kushirikiana na serikali ya Uingereza.