Serikali za Tanzania na India zimekubaliana kukuza ushirikiano katika sekta za kimkakati ambazo nchi hizo mbili zimeingia makubaliano rasmi ya ushirikiano kupitia uhusiano wa kihistoria, kidiplomasia na kimkakati uliopo baina ya mataifa hayo mawili.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi alipokutana kwa mazungumzo na Balozi wa India nchini Mhe. Balozi, Bishwadip Dey katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma tarehe 3 Oktoba, 2024.
Viongozi hao wamejadili juu ya kukuza ushirikiano katika sekta za kimkakati ambazo nchi hizo mbili zimekuwa zikishirikiana kwa karibu kuziendeleza hususan sekta ya biashara, uwekezaji, utalii, nishati, maji, afya na elimu.
Kwa upande wa Balozi Mbundi amempongeza Mhe. Dey kwa kuaminiwa kuiwakilisha Serikali ya India nchini kwakuwa ni mara ya kwanza anakutana naye kwa mazungumzo tangu aanze kuhudumu katika nafasi hiyo hapa nchini.
Pia ameeleza kuridhishwa na namna Serikali za Tanzania na India zinavyokuza ushirikiano kupitia ziara za Viongozi Wakuu wa nchi ambapo alirejea mafanikio yanayoendelea kupatikana kupitia ziara ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania nchini India iliyofanyika mwezi Oktoba, 2024 sambamba na Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja (JPC) kati ya Tanzania na India uliofanyika mwezi Julai, 2023 jijini Dar es Salaam.
Aidha, amesisitiza kuwa Tanzania imeweka dhamira ya kutumia kikamilifu fursa za kimkakati zilizopo kwa manufaa ya pande zote mbili ikiwemo; kutangaza vivutio vya utalii na kuwakaribisha wananchi wa India kutembelea maeneo hayo, kujenga uwezo wa watumishi wa Wizara na Serikali kwa ujumla kupitia ufadhili wa masomo ya muda mrefu na mfupi yanayotolewa nchini India katika masuala ya Akili Unde (Artificail Intelligence), diplomasia, uhandisi na mafunzo ya uongozi.
“Tanzania ina vivutio vya utalii vyenye sifa ya kipekee kulingana na uasilia wake, hivyo Mhe. Balozi katika ratiba yako ya ziara za mikoani unaweza kuanza kutembelea hifadhi ya Ngorongoro na Serengeti’’ alisema Balozi Mbundi.
Pia mikoa ya Mtwara, Lindi ( Kilwa), Pwani (Mafia), Ruvuma na Rukwa ina historia na utalii wa aina yake, pia mkoa wa Mara hususan Butiama ambako ndio nyumbani asilia kwa Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere utaweza kutembelea Makumbusho yake.
Fursa nyingine ni pamoja na: uwekezaji, kujenga uwezo katika masuala ya nishati ili kukidhi mahitaji ya matumizi ya wananchi nchini Tanzania sambamba na kukuza sekta ya maji ili wananchi waweze kufikishiwa huduma hiyo kwa karibu zaidi, sekta ya afya, sekta ya kilimo ambayo ni pamoja na zao la korosho na sekta ya biashara ambayo imeonesha mwenendo chanya wa ukuaji ambapo urari wa biashara kati Tanzania na India kwa takwimu za India umefikia takribani billion 8 sawa na shillingi za kitanzania trillion 21.5 na kuifanya Tanzania kuwa mbia namba mbili wa kibiashara na India kwa Afrika.
Naye Balozi Dey alisema tayari India imekuwa ikipokea Watanzania wengi wanaoingia katika nchi hiyo kwa ajili ya fursa mbalimbali na idadi hiyo imeendelea kukua zaidi hapa karibuni kufuatia kuhuishwa kwa ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na India. Vilevile Tanzania ni chaguo la watu wengi kutoka India kwa ajili ya mapumziko kwakuwa nchi hizo mbili zimekuwa zikishirikiana katika kujenga uwezo katika masuala ya utalii na ukarimu na kusaidia katika kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa elimu Mhe. Dey ameeleza kuwa India inatoa mafunzo ya Akili Unde katika vyuo vyake vya teknolojia vilivyopo nchini India na pia kwa upande wa Zanzibar tayari yametolewa mafunzo hayo kwa baadhi wa wanafunzi ambao wapo katika mpango wa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ili kushirikishana na kujenga uwezo wa teknolijia hiyo.
Balozi Dey pia ameeleza maendeleo ya ushirikiano katika sekta ya maji pamoja na nishati ambapo watumishi kutoka sekta hizo wanaendelea kupata mafunzo nchini India na akatolea mfano watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaendelea na mafunzo nchini humo kwa lengo la kujenga uwezo na kuinua utendaji katika sekta husika ambao utasaidia kupatikana kwa nishati ya uhakika kwa matumizi ya viwandani na nyumbani ikiwemo upatikanaji wa umeme wa jua.
‘’Ninafahamu Tanzania ina hifadhi kubwa ya rasilimali ya nishati hivyo India ipo tayari kushirikiana katika kujenga uwezo wa wataalamu na hata kuwekeza kwa kuwa ni eneo salama kwa uwekezaji kwa wananchi wetu ambao wengi wao wameshawekeza kwa muda mrefu na kuonesha kuridhishwa na mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania’’, alisema Balozi Dey.
Kadhalika, viongozi hao wamejadili fursa ya kukuza ushirikiano kati ya Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na mawaziri wa India katika sekta zenye maslahi kwa pande zote mbili.