Na Ashrack Miraji (Fullshangwe Media)
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, ameagiza vyombo vya usalama kuwatafuta na kuwachukulia hatua watu wote waliohusika na uharibifu wa miundombinu, ikiwemo vibanda vya kupumzikia watalii pamoja na mabomba ya maji katika Hifadhi ya Msitu Asilia Chome (Shengena) wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.
Ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake, alipoambatana na Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Same ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mkuu wa Wilaya hiyo Kasilda Mgeni, baada ya kupata taarifa za uharibifu huo katika hifadhi inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Mkuu wa Mkoa amesisitiza kwamba wahusika lazima wawe wamekamatwa ndani ya siku saba.
“Nimesikitishwa sana na baadhi ya Watanzania ambao bado hawatambui kwamba hii mali ni ya kwao. Kwenye eneo hili kuna mandhari nzuri, sehemu za kupumzika, na kunapendeza kabisa. Sasa wanatoka Watanzania wachache wanakwenda kuvunja mali ya Serikali. Hatuwezi kuvumilia vitendo vya namna hii,” alisema RC Babu.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amepiga marufuku kwa wachimbaji wadogo wa madini kuingia kwenye hifadhi hiyo bila vibali na kuendesha shughuli za kibinadamu, ikiwemo uchimbaji wa madini. Alisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kukiuka miongozo na sheria za uhifadhi, kwani eneo hilo ni maalum kwa ajili ya shughuli za utalii na utunzaji wa mazingira.
Sambamba na suala hilo, RC Babu ametembelea pia kaya za wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), ili kuona hali ya utekelezaji wa miradi hiyo. Mpango huo unalenga kusaidia baadhi ya kaya ambazo zimeingizwa kwenye mpango kwa lengo la kuziinua kiuchumi kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika jamii.