Na Farida Mangube, Morogoro
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezitaka taasisi za utafiti pamoja na zile zinazotoa mafunzo ya misitu kubuni mbinu na teknolojia rahisi zitakazosaidia wananchi wa vijijini kutumia rasilimali za misitu kwa njia endelevu. Lengo ni kuhakikisha wananchi wenye mitaji midogo na ujuzi wa kawaida wanapata fursa ya kunufaika na misitu kwa manufaa yao binafsi na kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Agizo hili lilitolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga (Mb), katika maadhimisho ya miaka 50 ya utoaji wa taaluma ya misitu yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA). Mhe. Kipanga aliitaka SUA kuhakikisha inaweka mikakati thabiti ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kwa kuwa sekta ya misitu ina nafasi muhimu katika maisha ya Watanzania na maendeleo ya taifa.
“Rasilimali za misitu zinaajiri zaidi ya watu milioni tatu, huku zikitoa maji, makazi na malisho ya wanyamapori, pamoja na kuhifadhi udongo na bayoanuwai. Aidha, misitu inasaidia kurutubisha hewa kwa kupunguza hewa ukaa, na pia kuchochea utalii wa kiikolojia,” alisema Mhe. Kipanga.
Naibu Waziri aliongeza kuwa sekta ya misitu pia imepewa kipaumbele katika mpango wa maendeleo ya taifa na malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa. Tangu kuanzishwa kwa Kitivo cha Misitu, Wanyamapori na Utalii hapo SUA, zaidi ya wataalamu wa misitu 2,630 wamehitimu na wanashiriki katika kusimamia rasilimali za misitu ndani na nje ya nchi.
Mhe. Kipanga aliendelea kueleza kuwa wataalamu hao wamechangia kwa kiasi kikubwa katika kutengwa kwa hekta milioni 48.1 za hifadhi za misitu na uanzishwaji wa hekta 582,729 za mashamba ya misitu ya kibiashara.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Raphael Chibunda, alisema kuwa chuo hicho kinajivunia sekta ya misitu, na kimejipanga kukifanya Kitivo cha Misitu kuwa kitivo cha umahiri kutokana na mchango wake katika ukanda wa SADC na Afrika Mashariki.
“Tuna kila sababu ya kujitathmini namna ya kudhibiti uharibifu wa misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema Prof. Chibunda.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala, alisisitiza kuwa Tanzania pamoja na mataifa mengine yameona matokeo chanya katika sekta ya misitu kutokana na uwepo wa Kitivo cha Misitu SUA, huku akiwataka vijana kuenzi jitihada za waasisi wa chuo hicho kama Hayati Edward Moringe Sokoine na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.