Na Waf – RUKWA
Madaktari 29 Bingwa na Bobezi wamewasili na kupokelewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Bw. Msalika Makungu kwa ajili ya huduma za kibingwa kwenye Halmashauri zote za mkoa kwa muda wa siku sita.
Bw. Makungu amewakaribisha madaktari hao leo tarehe 29 Septemba, 2024 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Makongoro Nyerere ambao watatoa huduma za kibingwa za Afya na kuwajengea uwezo watoa huduma mkoani humo.
“Tunapo kuja katika mkoa wa Rukwa kwa ajili ya kutoa huduma za afya na kuboresha uwezo kwa watumishi, tunajenga imani kwa wananchi dhidi ya Raisi wetu hivyo niwaombe kuifanya kazi hii kwa uaminifu na kwa bidii.”
Pia Bw. Makungu ameiaomba Wizara ya Afya kufanya programu hiyo kwa awamu zinazokuja iweze kufika mpaka katika ngazi ya msingi kwa vituo vya Afya kwani baadhi yake vipo mbali na hospitali za wilaya.
“Utaratibu uliowekea kwa kila robo niombe tupate walau nafasi ya kufika katika vituo vya Afya kwani yapo baadhi ya maeneo ambayo yapo mbali kidogo na Hospitali za Wilaya”, mesema Bw. Makungu
Nae Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Ramadhan Masusu amesema mkoa umejipanga vizuri kufanya matangazo kwenye Halmashauri zote wananachi wamesha anza kujiandikisha kwenye hospitali zilizo teuliwa na muitikio wa wananchi ni mkubwa.
“Hivyo ni matarajio yetu wanachi wa mkoa wa Rukwa wataenda kunufaika na ujio wa madaktari bingwa hawa kwani umewarahishia wananchi kutotumia gharama kubwa kufuata madaktari hospiti za Kanda na Taifa.” Amesema
Naye mwakilishi wa Wizara ya Afya Bw. Joachim Masunga ambae ni Afisa Programu Kutoka Idara ya Afya ya Uzazi Mama na Mtoto amesema malengo makubwa ya ujio wa Madaktari Bingwa hao ni kutoa huduma za kibingwa pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya mahala pa kazi ili kuweza kupunguza rufaa zisizo za lazima.