Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, ameziagiza idara ya Mifugo wilayani humo kuwachukulia hatua kali baadhi ya wakazi wanaoshindwa kuwafungia mbwa wao na kuwaacha wakizagaa mitaani, jambo linalosababisha madhara kwa wananchi na mifugo.
Chikoka alitoa agizo hilo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani yaliyofanyika wilayani Musoma. Inakadiriwa kuwa Halmashauri ya Wilaya hiyo ina mbwa wapatao 13,590 na paka 2,882.
Aidha, amesisitiza kuwasaka wamiliki wa mbwa 963 ambao mbwa wao wameachiwa huru mitaani na kusababisha athari kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kuwagonga, kuwag’ata, na kuua mifugo.
Kwa kushirikiana na wadau wa Animal Global Health Tanzania na Ifakara Health Institute, halmashauri hiyo ilianza mpango wa kutoa chanjo dhidi ya kichaa cha mbwa na paka kuanzia mwaka 2020 hadi 2024, hatua ambayo imeiwezesha kupata chanjo pamoja na vifaa muhimu.