Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANANCHI katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa kufika katika vituo vya kuandikishia wapiga kura ili kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura mapema kwa sababu zoezi linafanyika chini ya dakika tano.
Ushauri huo ulitolewa na Faraja Mbise, mkazi wa eneo la Chang’ombe, Kata ya Ihumwa, Halmashauri ya Jiji la Dodoma alipofanya mahojiano maalum baada ya kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura katika Kituo cha Shule ya Msingi Msuguri.
Mbise alisema “wito wangu kwa wananchi ambao bado hawajafika katika vituo vyao vya kujiandikisha, wafike mapema kwa sababu zaidi ya siku ya leo zitakuwa zimebaki siku mbili tu. Wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa sababu zoezi linaenda vizuri sana na kwa haraka. Ni zoezi ambalo halichukui hata zaidi ya dakika tano”.
Aidha, akiongelea utendaji wa maafisa uandikishaji, alisema kuwa wanafanya kazi vizuri. “Maafisa uandikishaji wamejipanga vizuri. Wanatoa huduma vizuri wanapokea watu vizuri sana wanauliza maswali vizuri na utaratibu ni mzuri, kuna upishano wa haki kati na wanawake kwa wanaume” alisema Mbise.
Kuhusu sababu za yeye kuwahi zaidi kituoni, alisema kuwa ana majukumu mengine ya kikazi. “Katika kituo nilichojiandikisha nilikuwa mwananchi wa tatu. Niliwahi mapema zaidi kujiandikisha ili kuhofia foleni hapo baadae ili niwe wa mwanzo kuhudumiwa na kuendelea majukumu mengine ya kazi. Hivyo, wananchi ambao bado hawajaenda vituoni kufanya hivyo, mapema na kuendelea na majukumu mengine kwa sababu muda wa kuhudumiwa ni mfupi sana” alisisitiza Mbise.
Leo ni siku ya tano tangu kuanza kwa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ukihusisha usajili wa wapiga kura wapya waliotimiza umri wa miaka 18, kurekebisha, kubadili taarifa au kuhama kituo chini ya kaulimbiu “Kujiandikisha, Kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora”