Eneo la maduka ya biashara na nyumba za makazi lililopo Gangilonga katika Manispaa ya Iringa limetemebelewa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah ambaye yupo katika ziara ya kutembelea Mikoa ya Shirika la Nyumba la Taifa iliyopo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kukagua miradi na kuhimiza utendaji kazi wenye kuleta tija kubwa
Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah akikagua maduka ya biashara eneo la Mlandege Manispaa ya Iringa na ameupongeza Mkoa wa Shirika Iringa kwa ubunifu walioufanya wa kujenga maduka hayo ya kisasa kwa muda mfupi ambayo sasa yaliingizia shirika mapato zaidi. Maduka hayo tisa kwa sasa yaliingizia Shirika mapato na kuwapa wananchi fursa za kufanya biashara
………………….
*Asisitiza wafanyakazi kulinda mafanikio yaliyopatikana
*Ahimiza uadilifu na uzalendo ili kulipatia Shirika tija kubwa
*Apongeza ubunifu wa Mkoa wa Iringa
*Aahidi kuendelea kupigania maslahi bora kwa wafanyakazi
Na Mwandishi Wetu, Iringa
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah, ameanza ziara ya kutembelea mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwa ni sehemu ya kukagua shughuli za Shirika, kuzungumza na wafanyakazi, na kuhimiza utendaji unaoleta tija.
Akiwasili mkoani Iringa na kukagua miradi mbalimbali iliyotekelezwa na mkoa huo, Bw. Abdallah alifurahishwa na ubunifu wa Mkoa wa Iringa katika kuongeza mapato ya Shirika. Alieleza kufurahishwa kwake na ujenzi wa maduka ya biashara kwenye viwanja vilivyokaa muda mrefu bila kuingiza mapato, akisema, “Hongereni sana kwa ubunifu huu wa kuyajenga maduka kwenye viwanja vya Shirika. Huu ni mfano wa kuigwa na kila mkoa.”
Akizungumza na wafanyakazi wa Mkoa wa Iringa, Bw. Abdallah aliwashukuru kwa shukrani walizompa kufuatia nyongeza ya mishahara, akiahidi kuendelea kupigania maslahi bora zaidi kwa wafanyakazi. Alieleza kuwa nyongeza hiyo ni juhudi za Shirika kuongeza mapato, akisema, “Mpira sasa uko kwenu. Mkifanya vizuri zaidi, ndani ya miezi sita nitahakikisha mnapata posho za nyumba na likizo, kama ilivyokuwa awali.”
Alisisitiza kuwa siri ya kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi ni kuzalisha faida zaidi, akibainisha kuwa Shirika limefanikiwa kuongeza mapato kwa asilimia 135. “Uadilifu na uchapaji kazi wenye tija ni muhimu ili tuendelee kupata faida na kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa siku zijazo,” alisisitiza.
Bw. Abdallah aliipongeza timu ya Mkoa wa Iringa kwa kukusanya kodi kwa asilimia 105, kubuni miradi ya maduka ya biashara, kufanya matengenezo ya nyumba, na kupunguza madeni ya kodi kwa asilimia 74. “Mmefanya kazi nzuri sana kwa kukusanya mapato kupitia miradi hii ya maduka. Haya maduka yanazalisha mapato makubwa zaidi kuliko majengo mengine ya ubia yenye gharama kubwa,” alisema.
Katika kuboresha taswira ya Shirika, Bw. Abdallah aliahidi kujenga jengo kubwa la kisasa kwa ajili ya biashara, ofisi, na makazi, ambalo pia litakuwa makao makuu ya ofisi za Shirika mkoani humo. Aliwahimiza wafanyakazi kuendelea kuwa wabunifu na kutozubaa kutokana na mafanikio waliyoyapata.
Aidha, aliwapongeza wafanyakazi kwa kurejesha nyumba ya Shirika iliyokuwa inamilikiwa kinyume na sheria. Alisema kuwa kuna majengo mengine ambayo yanaashiria kumilikiwa kinyemela, na akawahimiza wafanyakazi wafuatilie kwa umakini kuhakikisha yanarudishwa bila kuvunja sheria.
Meneja wa Shirika Mkoa wa Iringa, Bi. Esther Magese, alieleza kuwa lengo la mkoa ni kufuta kabisa madeni sugu na kuongeza mapato kupitia uwekezaji wenye tija. Alipendekeza ujenzi wa nyumba za kupanga na ofisi kutokana na fursa za utalii na kilimo zinazopatikana mkoani humo.
Kwa niaba ya wafanyakazi, Bi. Magese alimshukuru Mkurugenzi Mkuu kwa kuwapigania na kuhakikisha nyongeza ya mishahara. “Tunafurahia sana nyongeza hii, na tumejipanga kufanya kazi kwa bidii zaidi,” alisema.
Katika tukio la kushangaza, baada ya wafanyakazi kufundishwa kuhusu huduma kwa wateja na Meneja Habari na Uhusiano, Bw. Muungano Saguya, walipiga kura ya siri kuhusu kuridhika kwao na huduma za Shirika. Asilimia kubwa ya wafanyakazi waliridhika kwa asilimia 100, huku wachache wakiridhika kuanzia asilimia 85 na kuomba nyongeza zaidi ya maslahi, ikiwemo posho za nyumba na likizo.
Katika utafiti uliofanywa mwaka jana na Kampuni ya ABECC ya Chuo Kikuu Ardhi, ilibainika kuwa wafanyakazi wanaridhika na huduma za Shirika kwa asilimia 69.5, ikilinganishwa na asilimia 76 ya utafiti uliofanywa na Synovate mwaka 2014.