Na Ashrack Miraji – Fullshangwe Media
Mbunge wa Jimbo la Lushoto, mkoani Tanga, Shabani Shekilindi, ametoa onyo kali kwa watu wanaojaribu kuchonganisha wananchi na Serikali.
Shekilindi alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia kwenye mahafali ya wahitimu wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Mkurumuzi, kijijini Bombo, Kata ya Makanya, wilayani Lushoto.
“Ndugu zangu, sitokubali kikundi kidogo chenye tamaa ya madaraka kuwarubuni wananchi wa kata hii. Maendeleo makubwa yanatekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ni lazima tudumishe upendo na mshikamano,” alisema Shekilindi.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kuwa na shukrani kwa Rais Samia kwa juhudi zake katika kuleta maendeleo katika Jimbo la Lushoto, hususan Kata ya Makanya, ambayo imepokea zaidi ya Shilingi bilioni moja katika sekta ya elimu. Fedha hizo zimetumika kujenga Shule ya Sekondari ya Bombo A, na sasa ujenzi wa mabweni ya kisasa umeanza ili kuwasaidia wanafunzi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu.
Mbunge huyo pia alielezea jinsi Rais Samia alivyowezesha ujenzi wa kituo kikubwa cha afya katika kata hiyo, na amemuomba kujenga jengo maalum la huduma za Mama na Mtoto ili kupunguza changamoto wanazokutana nazo akina mama wanaohitaji huduma ya kujifungua na kliniki kwa watoto.
“Nashukuru Rais amekubali ombi hilo, na mwaka wa fedha 2024/2025 hatua za awali zitaanza. Haya yote ni matokeo ya mimi, mwakilishi wenu, kuyasemea bungeni. Leo, Makanya inaenda kuwa mji wa kisasa ukilinganisha na miaka ya nyuma,” alisema.
Shekilindi aliwaasa wananchi kuwa na shukrani, huku akiwahimiza kujitokeza kugombea na kuchagua viongozi wenye uwezo katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Aidha, aliwataka wazazi kuacha kupeleka watoto wao mijini kufanya kazi za ndani, badala yake wawapeleke shule ili wapate elimu itakayowanufaisha baadaye.
Mbunge huyo aliahidi kuwa atasaidia wanafunzi ambao hawana vifaa vya shule, na akawataka wazazi wenye changamoto za kulipa ada za sekondari kupeleka majina kwa mwenyekiti wa kijiji au diwani ili aweze kuwasaidia kulipa gharama hizo.
“Lengo letu ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030, Kata ya Makanya inakamilika kielimu kwa asilimia 100 kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo,” alisisitiza Shekilindi.