Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Francis Chalamila, akifuatilia mkutano huo.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila, akiwasilisha Mada
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Francis Chalamila,akikabidhi souvenir kwa Mhe. Balozi wa Tanzania – CHINA
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila,akizungumza na Bibi. Shamila Batohi – National Director of Public Prosecution ya Afrika Kusini.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila,akizungumza na Bw. Cheng Long – Senior Inspector Department of International Cooperation – China National Commission of Supervision.
………………
Tanzania inashiriki Kongamano la Tano la Kimataifa la Mashirikiano katika Mapambano Dhidi ya Rushwa, likiwa na lengo la kubadilishana uzoefu na utaalamu miongoni mwa Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa duniani.
Kongamano hilo la siku tano linahusisha washiriki kutoka mamlaka 219 za kuzuia na kupambana na rushwa kutoka nchi 121, ikiwemo Tanzania kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU). Moja ya vikao muhimu vya kongamano hili ni “High Level Forum”, ambako wakuu wa mamlaka hizo walitoa uzoefu wao kuhusu namna serikali zao zinavyokabiliana na rushwa kwa mafanikio.
Mada kuu zilizoangaziwa katika kongamano ni pamoja na:
1. Dira ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya rushwa (Global Vision)
2. Mfumo wa Kisheria na Kitaasisi (Legal and Institutional Framework)
3. Uendeshaji wa Mtandao wa GlobE (Operation of the GlobE Network)
4. Kujenga Ushirikiano wa Kimataifa (Building Cooperation)
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Francis Chalamila, aliwasilisha mada inayohusu Mfumo wa Sheria na Kitaasisi wa Tanzania katika Mapambano Dhidi ya Rushwa, akieleza namna ambavyo serikali imefanikiwa kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi. Alisema hatua kama kuanzishwa kwa Divisheni ya Mahakama Kuu inayoshughulikia kesi za rushwa na uhujumu uchumi ni miongoni mwa juhudi zinazowezesha mafanikio hayo.
Tanzania ni miongoni mwa nchi 70 zilizopata fursa ya kutoa wasilisho katika kongamano hilo, ambapo Bw. Chalamila aliwasilisha mafanikio ya Tanzania katika vita dhidi ya rushwa.
Mtandao wa GlobE, ulioanzishwa mwaka 2021, unalenga kubadilishana taarifa, uzoefu, na utaalamu miongoni mwa mamlaka za kupambana na rushwa. TAKUKURU ilijiunga na mtandao huu mwaka 2022 kama sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika vita dhidi ya rushwa.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Chalamila, alimtembelea Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Khamis Mussa Omar, mnamo Septemba 23, 2024, kwa lengo la kujitambulisha. Balozi Omar aliipongeza TAKUKURU kwa jitihada zake na kuhimiza kutumia vyema fursa za ushirikiano kati ya Tanzania na China katika vita dhidi ya rushwa.
Bw. Chalamila yuko Beijing, China, kushiriki Mkutano wa Tano wa Mtandao wa GlobE, unaoendelea kuanzia Septemba 24 hadi 27, 2024.