Na Ashrack Miraji (Fullshangwe Media) Kilimanjaro
Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amewapongeza wakazi wa Kitongoji cha Kiruwa, kilichopo Kijiji cha Ruvu Mbuyuni, Kata ya Mabilioni, kwa kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan katika sekta ya elimu.
Wakazi hao wamejitolea kwa hali na mali katika ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na ofisi za walimu katika Shule Mpya ya Msingi Kiruwa.
DC Kasilda alitoa pongezi hizo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, sambamba na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Alieleza kuwa juhudi zilizofanywa na wananchi wa eneo hilo ni mfano wa kuigwa, kwani serikali pekee haiwezi kutekeleza kila jambo kwa wakati mmoja bila ushirikiano kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali.
“Serikali imeshaagiza mjenge mpaka ngazi ya renta, mkifika hapo sasa mnaweza kuomba msaada zaidi. Kwa sababu Mkurugenzi ameona kazi nzuri, sasa itajumuishwa kwenye bajeti, na mimi nitaongeza nguvu ili fedha zije hapa,” alisema DC Kasilda.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Ruvu Mbuyuni, Vicent Mchomvu, alisema ujenzi wa shule hiyo ulianza mwaka 2019 kwa nguvu za wananchi, ambapo gharama ya mradi ilikadiriwa kuwa shilingi milioni 17.3.
Hadi sasa, zimetumika shilingi milioni 13.5, na ujenzi unaendelea hadi kufikia ngazi ya renta. Serikali itahakikisha inamalizia ujenzi huo kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo ili shule hiyo itoe huduma kwa jamii kama ilivyokusudiwa.
Naye Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same, Mohamed Ifanda, alieleza kuwa jitihada zinazofanywa na wananchi pamoja na serikali ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Rais Dkt. Samia ya kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana karibu na jamii.