Madereva Bajaji wa Kituo cha Bajaji Mlowo Wilaya ya Mbozi wametakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kujiepusha na ajali na madhara yake.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 26, 2024 na Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Wilaya ya Mbozi Mkaguzi wa Polisi Fidelia Kasongwa [DTO] alipokutana na madereva hao kwa lengo la kutoa elimu ya Usalama barabarani.
Nae Mkaguzi wa Polisi Kasongwa amesisitiza na kuwataka madereva hao kuzingatia sheria za usalama barabarani pindi wanapokuwa katika shughuli zao za usafirishaji abiria ikiwa ni pamoja na kutoendesha bajaji bila kuwa na leseni.
Vile vile amesisitiza na kuwataka madereva kuongeza umakini na kuheshimu watumiaji wengine wa barabara, kuheshimu misafara ya viongozi wa Kitaifa ambayo kimsingi ipo kisheria na taratibu za nchi na kuwataka kuwa na bima na kuwaelezea faida zake.
Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Julias Mkeni kutoka ofisi ya upelelezi wa makosa ya jinai aliwataka madereva hao kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi pindi inapotoke kukwazana na abiria au mwenzao na kwamba wanatakiwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili taratibu za kisheria zichukuliwe ikiwemo kufikishwa mahakamani.