Benki Kuu ya Tanzania inaendesha mafunzo kwa Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri kuhusu majukumu yake.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Gavana wa BoT, Bw. Emmanuel Tutuba, amewakaribisha washiriki wote na kueleza kuwa lengo kubwa la kufanya mafunzo hayo ni kuwaongezea uelewa kuhusu majukumu ya Benki Kuu.
“Mafunzo haya yana lengo la kuongeza uelewa wenu kuhusu kazi za Benki Kuu na uhusiano wake na kazi kubwa mnayoifanya katika Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri. Naamini kwamba kuongeza uelewa kuhusu mambo haya kutaimarisha ushirikiano kati ya taasisi zetu na kutuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi zaidi,” amesema Gavana Tutuba.
Amewaeleza wafanyakazi wa Sekretarieti hiyo kuwa jukumu la msingi la Benki Kuu ni kuunda na kutekeleza sera ya fedha ili kuhakikisha kuwa kuna utulivu wa bei na mazingira mazuri kwa ajili ya ukuaji endelevu wa uchumi wa nchi.
Aidha, ameongeza kuwa Benki Kuu ina majukumu mengine ikiwemo kuzihudumia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kusimamia akiba ya fedha za kigeni, kutengeneza na kusambaza sarafu ya nchi, kusimamia mifumo ya malipo na masoko ya fedha.
Aidha, ameihakikishia sekretarieti hiyo kuwa ukuaji wa uchumi wa nchi unaendelea kuimarika licha ya changamoto mbalimbali zinazoukabili uchumi wa dunia.
“Uchumi wa nchi yetu uko vizuri na sekta yetu ya fedha iko imara. Kupitia sera ya fedha na kwa kushirikiana na serikali kwenye sera za bajeti na uzalishaji, tumeweza kuwa na mfumuko wa bei wa takriban asilimia 3 kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, wakati ambao nchi nyingi duniani zilikuwa na mfumuko mkubwa wa bei,” amesema.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanafanyika katika ofisi za BoT, jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 26 hadi 28, Septemba, 2024 na yanawashirikisha wafanyakazi wa Sekretariati ya Baraza la Mawaziri wapatao 20.