Wadau wa Sekta ya Ununuzi wameaswa kutumia vyema mifumo ya ununuzi kwa njia ya kieletroniki hususan Moduli ya kuwasilisha malalamiko na rufaa inayopatikana katika mfumo wa NeST.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Tehama, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Priscus Kiwango alipokuwa akifunga kikao kazi cha siku nne cha majaribio ya Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia Malalamiko na Rufaa kieletroniki Jijini Dodoma.
Bw. Kiwango amesema kuwa anaamini kupitia kikao kazi hicho washiriki sasa hawatarudi tena nyuma, bali wataendelea kutumia moduli hiyo kuwasilisha malalamiko na rufaa kwani huokoa muda na gharama.
“Nawiwa kuamini ya kwamba katika kutekeleza zoezi la kuipitia moduli, mbali na kutoa maoni ya maboresho yanayopaswa kufanyika, mmeweza kujifunza namna moduli hii inavyofanya kazi, hususan kwa kuyaelewa vyema majukumu yenu ninyi kama taasisi nunuzi ambao ni wadau wakubwa katika matumizi ya moduli,” alisema Bw. Kiwango
Pamoja na mambo mengine, amewapongeza wataalamu kutoka Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) na Mamlaka ya Udhibiti ya Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kuandaa moduli hiyo ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa Umma kwa njia ya kielektroniki.
“Hii ni hatua kubwa katika historia ya ununuzi wa umma nchini, hususani katika kuhakikisha kuwa mchakato wa zabuni na malalamiko yanayotokana na michakato hiyo vyote vinafanyika kielektroniki, hongereni sana wataalamu,” alisema Bw. Kiwango.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mtendaji wa PPAA, Bi. Florida Mapunda amesema kikao kazi cha upimaji (User Acceptance Test) ya Moduli ya kuwasilisha na kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kieletroniki kilianza tarehe 23 – 26 Septemba 2024 na kimejumuisha washiriki kutoka taasisi 17 za Serikali pamoja na wazabuni kutoka kampuni mbalimbali.