Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Dk. John Simbachawene akizungumza katika kikao na Menejimenti ya Tume ya Ushindani FCC wakati alipotembelea ofisini hapo kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa FCC Bw. William Erik.
Mkurugenzi Mkuu wa FCC Bw. William ErikErik akimkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Dk. John Simbachawene wakati alipotembelea katika taasisi hiyo Leo Septemba 24, 2024.
……………..
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Dk. John Simbachawene, ameitaka Tume ya Ushindani (FCC) kuongeza juhudi katika udhibiti wa bidhaa bandia, hasa kipindi hiki ambacho maandalizi ya kuingia kwenye soko huru la biashara barani Afrika yanaendelea. Hii ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kukuza uchumi na biashara nchini.
Akizungumza jana alipokuwa akitembelea ofisi za FCC jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza tangu kuteuliwa kwake, Simbachawene alisisitiza umuhimu wa kuimarisha udhibiti kwenye maeneo ya mipakani. Alisema kuwa tume hiyo itakabiliwa na changamoto kubwa zaidi ya bidhaa bandia mara baada ya kuanzishwa kwa soko hilo, hivyo ni muhimu kuchukua hatua za mapema.
“Itakuwa ni changamoto kubwa kudhibiti bidhaa bandia mara tu baada ya soko huria la biashara Afrika kufunguliwa, hivyo ni muhimu mjipange vizuri mapema,” alisema.
Ameitaka FCC kuongeza maofisa na kuongeza jitihada katika majukumu yao ya kulinda walaji, kulinda bidhaa zinazozalishwa nchini, na kuhakikisha uchumi wa taifa unakuwa imara dhidi ya athari za bidhaa bandia.