Na Ashrack Miraji (Fullshangwe Media), Lushoto Tanga
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Dkt. Batilda Buriani, ameagiza kuwa Tamasha la Usambara Tourism Festival 2024 litumike kama njia ya kuhamasisha wananchi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.
Akiwa ameambatana na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Dkt. Batilda alitoa agizo hilo alipokuwa wilayani Lushoto kukagua maandalizi ya Tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika tarehe 21-22 Septemba 2024 katika viwanja vya Nyerere Square.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Batilda alisema kuwa Tamasha hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na watu wengi kutoka sehemu mbalimbali za Lushoto na Tanzania kwa ujumla. Hivyo, alisisitiza kuwa ni fursa muhimu ya kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.
“Kama mnavyojua, taifa letu kwa sasa liko katika maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Jana tarehe 16 Septemba 2024, Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, alitangaza mipaka na maeneo ya utawala kwa nchi nzima, na mimi nikaweka wazi maeneo ya Mkoa wa Tanga,” alisema Dkt. Batilda.
Aliendelea kusisitiza kuwa tamasha hilo ni jukwaa sahihi kwa kuelimisha na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huo, akisisitiza kuwa mabango na matangazo ya tamasha yahusishe kauli mbiu inayosema, “Serikali za Mitaa Sauti ya Wananchi, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi.”
Katika hatua nyingine, Dkt. Batilda alipokea taarifa ya maandalizi ya Tamasha hilo kutoka kwa Kamati ya Maandalizi inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mhe. Zephania Sumaye. Baada ya kupokea taarifa hiyo, alikagua maendeleo ya maandalizi, huku akibainisha kuwa mgeni rasmi wa tamasha hilo anatarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Dotto Biteko.
Tamasha la Usambara Tourism Festival 2024 limeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, likiwa na lengo la kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kutangaza utalii wa ndani.