Takribani watu sita wanahofiwa kufa maji baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama ndani ya Ziwa Victoria, mkoani Mara. Tukio hili limetokea Septemba 15, 2024, majira ya saa 1 jioni, wakati kundi hilo likitoka kwenye sherehe ya harusi eneo la Mwiruruma, kata ya Ilamba, wilayani Bunda.
Kwa mujibu wa mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Mapambano Kasala, aliyekuwepo kijiji cha Igundu, mtumbwi huo ulikuwa umesheheni zaidi ya watu 20. Inadaiwa kuwa mtumbwi ulizama kutokana na uzito mkubwa wa watu waliokuwepo.
“Tulifanikiwa kuokoa baadhi ya watu wakiwa hai, lakini mwili wa mwanamke mmoja ulipatikana jana hiyo hiyo, ukiwa umenaswa kwenye nyavu za nanga. Zaidi ya watu sita bado hawajapatikana hadi sasa,” alisema Kasala.
Kundi hilo lilikuwa limetoka kusherehekea harusi upande wa bibi harusi na walikuwa wakielekea nyumbani kwa bwana harusi kwa maandalizi ya sherehe nyingine iliyopangwa kufanyika leo, Septemba 16, 2024.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk. Vicent Naano, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na amesema kuwa mpaka sasa watu tisa wameokolewa wakiwa hai. “Tayari mwili mmoja umepatikana na jitihada za kuwasaka watu wengine sita zinaendelea,” alisema Dk. Naano.
Aliongeza kuwa juhudi za uokoaji zinaendelea na tayari ameelekea eneo la tukio ili kusimamia zoezi hilo kwa karibu.