Na Na John Bukuku
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ametaja sekta ya ardhi kuwa kinara wa vitendo vya rushwa katika mkoa huo na ameahidi kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuhakikisha rushwa haiwi kikwazo kwa wakazi wa Arusha kupata haki zao.
Makonda aliyasema hayo hivi karibuni alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, aliyemtembelea ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha na kumpongeza kwa juhudi zake katika kupambana na rushwa mkoani Arusha.
“Katika sekta ya ardhi, najua umesikia kilio kikubwa hapa. Hii ni sekta ambayo watu wanaonekana kama wanawajibika kudai rushwa ili kupata huduma. Hata kwa vibali vya ujenzi, unakuta mtu anafuatilia kibali kana kwamba anafanya kosa. Mwisho wa siku, wengine wanajenga bila vibali, na matokeo yake ni ujenzi holela,” alisema Makonda.
Aliongeza kuwa ni lazima kuhakikisha kuwa hakuna jambo linalokwamisha vijana wa TAKUKURU kufanya kazi zao kikamilifu. “Tunataka haki itendeke, mtu asionewe, na watu wasiishi kwa dhana kwamba bila rushwa hawawezi kufanikisha jambo,” alisisitiza Makonda.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Chalamila, aliahidi kuongeza maafisa zaidi mkoani Arusha ifikapo Novemba mwaka huu, ili kuongeza kasi katika mapambano dhidi ya rushwa, kufuatia ombi la Makonda alilolitoa mwezi Mei 2024.
Aidha, Chalamila alimwomba Makonda kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu kwa umakini mkubwa, akibainisha kuwa kupatikana kwa viongozi waadilifu ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya mkoa wa Arusha.
“Uchaguzi huu wa serikali za mitaa ni muhimu sana, ni maandalizi ya uchaguzi mkuu mwakani. Viongozi watakaochaguliwa mwaka huu watahusika moja kwa moja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa nchi nzima. Ni muhimu tuhakikishe tunapata viongozi safi, ambao wamechaguliwa kwa haki, ili waweze kufuatilia utekelezaji wa miradi hii kwa ufanisi na kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana,” alisema Chalamila.
Aliahidi kuongeza maafisa wa TAKUKURU mkoani Arusha kabla ya Novemba 27, mwaka huu, ili kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanyika bila dosari za rushwa. “Tumesikia ombi lako, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, na tunalichukua kwa uzito mkubwa,” alihitimisha Chalamila.