Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (WaPili kushoto) akitoa maelekezo kwa Mhandisi Mshauri kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) Kitengo cha TECU, Simon Makala (WaNne kulia) alipokagua ujenzi wa barabara ya Ruangwa – Nanganga (Km 53.2) kwa kiwango cha lami na daraja la Lukuledi lenye urefu wa mita 60 Septemba 14, 2024 mkoani Lindi.
Mhandisi Mshauri kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) Kitengo cha TECU, Simon Makala akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (WaPili Kushoto) wakati Naibu Waziri huyo alipokagua ujenzi wa barabara ya Ruangwa – Nanganga (Km 53.2) kwa kiwango cha lami na daraja la Lukuledi lenye urefu wa mita 60 Septemba 14, 2024 mkoani Lindi.
Mhandisi Mshauri kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) Kitengo cha TECU, Simon Makala akieleza hatua za ujenzi zilizofikiwa katika daraja la Lukuledi kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (WaPili kushoto) wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Ruangwa – Nanganga (Km 53.2) kwa kiwango cha lami na daraja hilo lenye urefu wa mita 60 mkoani Lindi.
Kazi za usukaji wa nondo katika darajala Lukuledi, mkoani Lindi lenye urefu wa mita 60 zikiendelea. Daraja hilo limefika asilimia 32. 7 na linatarajiwa kukamilika Februari, 2025.
Muonekano wa barabara ya Ruangwa – Nanganga (Km 53.2) kwa kiwango cha lami ambayo imefika asilimia 81 na inatarajiwa kukamilika Februari, 2025.
………………………..
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amemtaka Mkandarasi M/s China Railway 15 Bureau Group Corporation anayejenga barabara ya Ruangwa – Nanganga (Km 53.2) kwa kiwango cha lami kuhakikisha ujenzi wake unakamilika ifikapo Februari mwakani.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, Septemba 14, 2024 Naibu Waziri Kasekenya amaesema tayari ujenzi wa barabara hiyo umefikia asilimia 81 na kusisitiza asilimia 19 zilizobaki zikamilishwe katika kipindi cha miezi mitano iliyobakia.
“Hakikisheni kazi zote za madaraja zinazoweza kuathiriwa na mvua zinakamilika katika kipindi hiki ili mvua zitakapoanza kunyesha ujenzi usisimame na hivyo kufikia lengo la kukamilisha barabara yote”, amesema Kasekenya.
Ameongeza kuwa tayari Mkandarasi amepatikana wa sehemu ya kwanza ya barabara hiyo kutoka Nachingwea – Ruangwa na ujenzi wa sehemu hiyo utaanza wakati wowote kuanzia sasa.
“Barabara hii inaanzia Nachingwea- Ruangwa – Nanganga (Km 106), hivyo kukamilika kwa sehemu ya Ruangwa – Nanganga kutakuwa kumeifungua takriban nusu ya barabara hii, wakati ujenzi wa Nachingwea – Ruangwa ukiendelea wananchi tumieni fursa ya ujenzi wa barabara hii kupata ajira, ujuzi na kuzalisha mazao yatakayosafirishwa kwa barabara hii itakapokamilika”, amesisitiza Kasekenya.
Amemtaka Mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana katika ujenzi wa daraja la Lukuledi lenye urefu wa mita 60 na kuhakikisha eneo hilo linapitika wakati wote wakati ujenzi ukiendelea.
Aidha, Naibu Waziri Kasekenya amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho kupata wakandarasi watakaojenga madaraja yaliyoathiriwa na mvua kubwa iliyonyesha mwaka huu katika barabara ya Mingoyo – Dar es Salaam ili kuyajenga katika ubora utakaoweza kuruhusu maji kupita kwa urahisi na kulinda barabara hiyo.
Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) Kitengo cha TECU, Simon Makala amesema watahakikisha wanamsimamia kikamilifu Mkandarasi ili kazi zote zinazoweza kuathiriwa na mvua zikamilike kabla ya mvua kuanza.
Amefafanua kuwa makalvati madogo 54 na makubwa 37 tayari yamekamilika huku daraja la Lukuledi ujenzi wake ukifikia asilimia 32.7
Naibu Waziri Kasekenya anaendelea na ziara yake ya siku Tano katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo anakagua miundombinu ya barabara na madaraja.