Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria imeanza kuchunguza mbinu za kutumia lugha rahisi na zinazoeleweka kwa jamii zinazozunguka Bonde la Mto Mara ili kuhakikisha mafanikio katika uhifadhi wa bonde hilo kwa maslahi ya wananchi na Jumuiya kwa ujumla.
Kauli hiyo ilitolewa na Dk. Masinde Bwire, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, wakati wa kongamano la utafiti wa kisayansi lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Masai Mara, Kaunti ya Narok, nchini Kenya.
Dk. Bwire alieleza kuwa matumizi ya lugha zinazofanana katika maeneo yanayozunguka bonde hilo yatasaidia kurahisisha juhudi za kulinda rasilimali za bonde hilo na kuwawezesha wanajamii kuelewa na kushiriki kikamilifu katika jitihada za uhifadhi.
“Imekuwa changamoto kwa jamii kutofahamu lugha zinazotumika katika tafiti mbalimbali. Hivyo, endapo kutakuwa na matumizi ya lugha mama za jamii husika, itarahisisha uelewa na ushirikiano katika juhudi za kulinda bonde. Kama kamisheni, tumeanza kulifanyia kazi hili na tunalenga kupata tafsiri sahihi kutoka kwa wataalamu wetu,” alisema Dk. Masinde Bwire.
Kwa upande wake, Mwanazuoni Profesa Patrick Lumumba alisema kuwa tafiti nyingi zimeandikwa kwa lugha ngumu, jambo linalozuia jamii zinazozunguka bonde hilo kuzifahamu kikamilifu.
“Ni lazima tutumie lugha inayoeleweka. Tunahitaji kuwa na misamiati inayofahamika katika mitaa na vijiji vinavyozunguka bonde hilo. Maneno magumu kama ‘baianua’ na ‘ikolojia’ yanapaswa kutafsiriwa kwa lugha za jamii husika ili yaeleweke vyema,” alisisitiza Prof. Patrick Lumumba.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanal Evans Mtambi, alieleza kuwa kila mwananchi ana jukumu la kulinda mazingira na wanyama walioko katika maeneo husika, akisisitiza umuhimu wa ushiriki wa kila mmoja katika jitihada za kuhifadhi bonde la Mto Mara.