Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamepinga vikali maandamano yaliyotangazwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yanayopangwa kufanyika Septemba 23, 2024, yakilenga kushinikiza kurejeshwa kwa watu waliopotea katika mazingira ya kutatanisha.
Wakizungumza na Fullshangwe Media, wananchi hao wamesema kuwa amani iliyopo nchini ni ya kujivunia na haiwezi kupotezwa kwa urahisi. Wanaamini kwamba kuna mataifa mengi ambayo yanakabiliwa na changamoto za kukosa amani, hivyo Tanzania inapaswa kujivunia utulivu uliopo.
Nasi Ngayoma, mmoja wa wananchi hao, alisema, “Tanzania siku zote imekuwa nchi ya amani, na ni vyema jamii ikaendelea kujivunia hali hiyo. Dunia nzima inatushangaa kwa jinsi tunavyoishi kwa utulivu bila kugombana, si tu kati yetu wenyewe, bali hata na majirani zetu.”
Ngayoma aliongeza kuwa CHADEMA wamepewa uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, lakini bado hawaridhiki. “Rais Samia amewapa uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara, lakini wanataka zaidi na hata wanamkashifu. Wanataka kuharibu amani hii kwa sababu zao binafsi,” alisema Ngayoma.
Chande Said , naye, alieleza kuwa maandamano yaliyopangwa hayana tija kwa taifa, kwani Rais Samia ameleta mabadiliko makubwa ya uhuru wa kisiasa ukilinganisha na miaka ya nyuma. “Sioni ulazima wa maandamano hayo. Ni muhimu vijana wawe makini na kauli zinazotolewa na viongozi wa juu, kwani mara nyingi ni matakwa ya kibinafsi,” alisema Sembinkugwa.
Kwa upande wake, Said Maona, fundi cherehani, alisema kuwa maandamano hayo yanakusudia kuchafua taswira ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa madai ya utekaji, jambo ambalo alilipinga. “Inawezekana wanajiteka wao wenyewe. Serikali inapaswa kuangalia suala hili kwa makini, hasa tunapoelekea uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unapaswa kufanyika kwa amani,” alisema Maona.
Mwanamke mwingine, ambaye hakutaka jina lake kutajwa, alisema kuwa kitendo cha CHADEMA kumtukana Rais Samia Suluhu Hassan ni cha kuudhalilisha wanawake wote. “Nimesikitishwa sana na kitendo hiki. Kama wanamtukana Rais Samia ambaye ni mwanamke, je wakichukua madaraka itakuwaje kwa wanawake wengine? Hili suala halipaswi kufumbiwa macho, na sheria inapaswa kuchukua mkondo wake,” alisema.
Aliendelea kwa kuomba serikali ichukue hatua dhidi ya wote waliotoa kauli za matusi dhidi ya Rais Samia, akisema kuwa kudhalilishwa kwa mwanamke mmoja ni sawa na kudhalilisha wanawake wote duniani. Alitoa wito wa kufutwa kwa chama hicho kama hakitachukua hatua za kurekebisha tabia zake.
Mwisho, wananchi hao waliitaka serikali kuhakikisha amani inatawala katika kipindi hiki, na kuonya kuwa maandamano hayo yanaweza kuhatarisha utulivu wa nchi.