NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Emmanuel Nchimbi amelitaka Taifa kuungana kulaani utekaji na mauaji yanayoendelea nchini ikiwemo mauaji ya kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mohammed Kibao tukio ambalo limewatia hofu watanzania.
Akizungumza na wahariri pamoja na waandishi wa habari leo Septemba 13, 2024 jijini Dar es Salaam Dkt. Nchimbi, amesema kuwa matukio ya utekaji na mauaji hayawezi kupuuzwa, huku akiwataka watanzania kutoa muda kwa Jeshi la Polisi kufanya uchuguzi ili kubaini wahusika.
Dkt. Nchimbi amesema kuwa matendo ya utekaji yanafanywa na watu wenye nia mbaya ya kufarakanisha taifa, kwani matukio hayo yanaleta taswira mbaya kwa CCM hivyo hayapaswi kupewa ushirikiano.
“Tayari matendo hayo yanafanya raia wasiwe na imani na Jeshi la Polisi, vitendo hivyo vikiendelea vinaathiri usalama na ustawi wa nchi kwa ujumla, ni muhimu sisi pamoja na wapinzani kushirikiana ili tusiwape genge la watekaji ushindi, genge linataka kutufarakanisha” amesema Dkt. Nchimbi.
Kiongozi huyo amesema CCM inaunga mkono kauli ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutaka uchunguzi ufanyike. “Niseme kuwa CCM imekerwa kweli kweli na jambo hili… Genge hili la watekaji linaweza kuwa popote, ndani ya CCM, Polisi au hata Chadema. Muhimu ni kuacha uchunguzi wa kina ufanyike, na majibu yake yapatikane ili hatua zichukuliwe”.
Kuhusu hoja ya CHADEMA ya kutaka uchunguzi uongozwe na makachero kutoka mashirika ya kijasusi ya kimataifa kama Scotland Yard ya Uingereza, Dkt. Nchimbi amesema CCM itaiunga mkono serikali kama itaona umuhimu wa kushirikisha mashirika ya kimataifa.
Dkt. Nchimbi amesema kuwa misimamo ya Chadema ya kutaka Rais Dkt. Samia ang’oke madarakani haiwezekani kwa kuwa yupo madarakani kikatiba na ataondoka pale tu muda wake kikatiba utakapotamatika.
Dkt. Nchimbi amesema kuwa watu wenye nia mbaya wamekuwa wakiendesha magenge ya uhalifu wakiwa na nia mbaya ya kukigombanisha CCM na wananchi.
Amesema kuwa ni wajibu wa CCM kwa kushirikiana na vyama vya upinzani kuhakikisha genge la watekaji halifanikiwi katika mkakati wa kuwagombanisha.
“Kosa kubwa tutakalofanya ni kuwapa ushindi genge la watekaji, sisi CCM tumekataa kushiriki katika majadiliano ambayo hayana tija” amesema Dkt. Nchimbi.
“Nchi hii ya watanzania wote na tunao wajibu wa kipekee wa kuijenga nchi yetu, watoto wetu na wajukuu wetu wanakuja kupata Taifa nzuri na madhubuti ” amesema Dkt. Nchimbi.
Amesema kama CCM watafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha demokrasia katika nchi inaendelea kushamili pamoja na kuwepo kwa mahusiano mzuri ya vyama na vyama katika kuimarika umoja na kuijenga nchi.
“Tunaamini katika mazungumzo, ushirikiano, wao na sisi katika kulijenga Taifa lenye umoja na mshikamano, tupo tayari kushirikiana nao” amesema Dkt. Nchimbi.