Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), Bw. James Sando akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) pembezoni mwa Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki Jijini Arusha
Naibu Katibu Mtendaji wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA), Bi. Florida Mapundaa akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) pembezoni mwa Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki Jijini Arusha
……………..
Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeanzisha mkakati wa kutoa elimu kwa wazabuni katika kanda zote nchini, ili kuimarisha ushiriki wao katika michakato ya ununuzi wa umma. Hii ni sehemu ya jitihada za mamlaka hiyo kuwafikia wadau wake muhimu na kuwaelimisha juu ya haki zao na taratibu za kuwasilisha rufaa pale wanapokuwa hawajaridhishwa na mchakato wa zabuni.
Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando, alieleza mkakati huo wakati akizungumza na waandishi wa habari pembezoni mwa Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki, lililofanyika Jijini Arusha. Alisema lengo ni kuwafikia wazabuni katika kanda nne ambazo bado hazijapatiwa elimu ya kutosha kuhusu namna ya kuwasilisha malalamiko yao.
“Kwa mwaka wa fedha 2024/25, tumejipanga kuzifikia kanda za kati, kaskazini, nyanda za juu kusini, na kusini, ili kuhakikisha wazabuni wengi zaidi wanapata elimu ya namna ya kushiriki na kuwasilisha rufaa kwenye michakato ya zabuni za umma,” alisema Bw. Sando.
Aidha, Naibu Katibu Mtendaji wa PPAA, Bi. Florida Mapunda, alielezea manufaa ya mfumo mpya wa kielektroniki wa kuwasilisha rufaa, akisema kuwa mfumo huo umesaidia kupunguza muda na gharama. Kwa mujibu wa Bi. Mapunda, moduli hiyo mpya itawezesha uwazi na ufuatiliaji wa karibu wa rufaa kutoka kwa wazabuni, huku ikiboresha uwajibikaji kwenye michakato ya utoaji haki.
“Mfumo huu unampa mzabuni uwezo wa kufuatilia hatua kwa hatua jinsi rufaa yake inavyoshughulikiwa, hali ambayo itasaidia kujenga imani kwa wazabuni katika mfumo wa ununuzi wa umma,” alisema Bi. Mapunda.
Kongamano hilo lililowaleta pamoja wadau zaidi ya 1,500 wa ununuzi wa umma kutoka ndani na nje ya nchi, lilibeba kauli mbiu ya “Matumizi ya Dijitali kwa Ununuzi wa Umma Endelevu,” likilenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika kuboresha michakato ya ununuzi wa umma.