10 Septemba 2024, Arusha:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewasisitiza wadau wa sekta ya ununuzi kuzingatia na kutumia ipasavyo huduma za hali ya hewa wakati wa kupanga na kutekeleza miradi ya ujenzi nchini.
Akizungumza katika Jukwaa la 16 la Ununuzi la Afrika Mashariki lililofanyika AICC, Arusha, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa TMA, Dkt. Hamza Kabelwa, alieleza kuwa huduma za hali ya hewa ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na kuleta thamani ya fedha. Alisema, “Miradi mingi ya ujenzi imeathiriwa na hali mbaya ya hewa, hivyo ni muhimu kwa wadau wa ununuzi kuzitumia huduma hizi wakati wa kupanga na kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi yao.”
Pamoja na hayo, Dkt. Kabelwa aliwakumbusha washiriki kwamba huduma hizi zinahitaji kuchangiwa gharama kidogo ili kuwezesha uendeshaji bora. Alieleza kwamba, mabadiliko ya sheria za TMA yaliyopendekezwa kwenye bajeti ya mwaka 2024/25 yataongeza ufanisi na usalama katika miradi ya ujenzi nchini.
TMA pia ilibainisha kuwa utoaji wa huduma bora za hali ya hewa unahitaji uwekezaji wa miundombinu ya kisasa na gharama kubwa za uendeshaji. Hivyo, ili kuhakikisha usalama na tija katika miradi ya ununuzi, wadau wanahimizwa kushirikiana na TMA kwa kuchangia gharama za huduma hizo maalum.