Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura akifungua semina ya waandishi wa habari kuhusu magonjwa yasiyoyakuambikzwa inayofanyika kwenye hoteli ya Protea Courtyard Upanga jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA, Bi. Tike Mwambipile akifafanua mambo kadhaa katika semina hiyo.
Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano, Afrika kutoka Global Health Advocacy Incubator (GHAI), Bobi Odiko akifafanua mambo kadhaa katika semina hiyo inayofanyika kwenye hoteli ya Protea Upanga jijini Dar es Salaam.
………………..
Na Sifras Kingamkono, Dar es Salaam
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, amewataka waandishi wa habari kuzingatia maadili na ubora katika kazi zao huku wakiendelea kuzingatia sheria na kulinda hadhi ya watu. Akizungumza katika semina kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza iliyoandaliwa na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Sungura amesisitiza umuhimu wa kuandika habari zenye ushawishi na zinazochochea nidhamu katika tasnia ya uandishi wa habari.
Sungura amefafanua kuwa MCT itaendelea kushirikiana na wadau kama TAWLA pamoja na vyombo vya habari kuhakikisha habari zinazohusiana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza zinafika kwa umma kwa lengo la kuhamasisha mapambano dhidi ya magonjwa hayo.
Aidha, Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano, Afrika kutoka Global Health Advocacy Incubator (GHAI), Bobi Odiko, ameipongeza TAWLA kwa juhudi zake za kuandaa mafunzo ya lishe bora kwa waandishi wa habari. Odiko amesema kuwa mafunzo hayo yamejikita katika kuboresha sera na utafiti ili kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi kuhusu vyakula bora, pamoja na kuleta mabadiliko ya sera na sheria zinazohusiana na lishe.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA, Bi. Tike Mwambipile, ameongeza kuwa ukosefu wa mazoezi ni mojawapo ya sababu kubwa zinazochangia magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile magonjwa ya moyo na kisukari. Amesema kuwa gharama kubwa zinazotumika kutibu magonjwa haya zinaweza kupunguzwa endapo jamii itahimizwa kufanya mazoezi na kutumia vyakula visivyo na kemikali. Pia alitoa wito kwa serikali kuweka sheria na sera zinazodhibiti uzalishaji wa vyakula salama na kutoa mwongozo wa uwajibikaji kwa wafanyabiashara.