Waziri wa Uvuvi, Abdallah Ulega, ameweka wazi fursa kubwa zinazokuja kwa sekta ya uvuvi Tanzania kufuatia mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, ambapo Tanzania imeibuka kama moja ya nchi zinazofaidika na ushirikiano huo. Akizungumza hivi karibuni katika mkutano uliofanyika nchini China, Waziri Ulega alieleza kuwa sekta ya uvuvi na mifugo ilipewa kipaumbele cha kipekee, na mipango mbalimbali ya maendeleo kujadiliwa kwa kina.
Waziri Ulega alieleza kuwa mojawapo ya mafanikio makubwa ya mkutano huo ni nafasi ya kuendeleza sekta ya uvuvi kupitia uwekezaji mpya wa kampuni mbili za Kichina ambazo zimeonyesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania. Kampuni moja itajikita katika uvuvi wa maji baridi, huku nyingine ikilenga uvuvi wa maji chumvi. “Hizi kampuni zitaleta teknolojia mpya, mitaji, na mafunzo ya jinsi ya kuongeza uzalishaji wa samaki kwa njia bora na endelevu,” alisema Ulega, akiongeza kuwa mazungumzo hayo yalipata msukumo mkubwa kutokana na uhusiano mzuri kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa China.
Waziri Ulega pia aliweka wazi kuwa teknolojia na mitaji itakayoletwa na makampuni hayo yatatoa fursa kwa vijana wa Kitanzania, hususan wale walioko kwenye Programu za *BBT* (Building a Better Tomorrow). Vijana hao watapata nafasi ya kujifunza kutoka kwa wataalamu wa China kuhusu njia bora za uzalishaji wa samaki, huku wakilenga soko kubwa la Kichina ambalo sasa linahitaji bidhaa kutoka Tanzania.
Aidha, mpango wa kubadilishana uzoefu utawezesha vijana wa Kitanzania kwenda China kujifunza moja kwa moja kutoka kwa wataalamu waliobobea katika uvuvi. “Kuona ni kuamini,” alisema Ulega, akisisitiza kuwa fursa hii itawezesha vijana kujifunza mbinu bora za uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa za samaki.
Waziri Ulega pia alisisitiza umuhimu wa Watanzania kuchangamkia fursa zinazotokana na ushirikiano huu, siyo tu katika uvuvi, bali pia katika sekta ya mifugo. Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kufungua masoko mapya, ikiwemo soko la nyama ambalo sasa linaenda kuuzwa nchini China.
Uhusiano wa muda mrefu kati ya China na Tanzania unaendelea kuzaa matunda, huku ushirikiano wa kiuchumi ukiimarika zaidi kupitia fursa hizi mpya za kibiashara. “China inataka kuifanya Tanzania kuwa kielelezo cha mafanikio katika ushirikiano huu wa kimkakati,” alihitimisha Ulega.
