Mkurugenzi Mkuu wa PPRA ,Dennis Simba akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha kuhusu kongamano hilo.
……..
Happy Lazaro, Arusha.
Rais wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgenirasmi katika kongamano la 16 la ununuzi wa umma la Afrika Mashariki litakalofanyika kesho katika ukumbi wa mikutano Aicc mkoani Arusha .
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo ,Mkurugenzi Mkuu wa PPRA ,Dennis Simba amesema kuwa ,zaidi ya washiriki 1,000 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo huku kauli mbiu ikiwa ni “ununuzi endelevu wa kidigitali “.
Simba amesema kuwa, tayari maandalizi yameshakamilika na wameshaanza kupokea washiriki nchi nane za Afrika Mashariki na wengine kutoka nje ya jumuiya ya Afrika Mashariki .
Amesema kuwa,washiriki wanatarajiwa kujadili kwa siku nne kuhusu msukumo wa kufanya ununuzi wa umma kidigitali ,na hatua hii inaipa nafasi zaidi nchi yetu ambayo imepiga hatua kubwa mbele kwa kujenga mfumo wa NEST ambao utazinduliwa katika ufunguzi wa kongamano hilo.
“Tukio hilo litaongeza hamasa kwenye juhudi alizozianzisha mheshimiwa Rais kwa kuitangaza nchi yetu na kuhamasisha ongezeko la watalii nchini,kwa kuzingatia kuwa Arusha ni kitovu cha sekta ya utalii.”amesema Simba.