Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa BANK OF AFRICA-TANZANIA, Hamza Cherkaoui, akiongea na wateja wa benki hiyo waliohudhuria warsha ya kuwajengea uwezo iliyoandaliwa na Benki hiyo na kufanyika mjini Kahama mkoani Shinyanga.
Mmoja wa Wateja wa Bank of Africa Tanzania Nzella J. Nzella, akichangia mada wakati wa warsha ya kuwajengea uwezo wateja wa Benki hiyo iliyofanyika mjini Kahama.
……………..
Bank of Africa Tanzania , imeendesha semina kwa wajasiriamali wa Kahama mkoani Shinyanga , kupitia kauli mbiu ya “TUKUE PAMOJA” inayodhihirisha mkakati wake wa kusaidia Wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) nchini Tanzania katika kufanikisha ukuaji wa kifedha na kuimarika kwa biashara zao.
Semina hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Planet mjini Kahama, ililenga kutoa elimu ya kifedha kwa kina, ambapo mada mbalimbali za kibiashara zilifundishwa na kujadiliwa ikiwemo uwasilishaji wa rekodi za biashara, masuala ya kodi, na mikakati ya kuongeza uwezo wa huduma za kibenki ili kuchochea ukuaji wa mtaji.
Akiongea wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa BANK OF AFRICA-TANZANIA, Hamza Cherkaoui alisema “Katika mpango wetu wa kimkakati wa miaka mitatu, sekta hii nyeti ya wajasiriamali imepewa kipaumbele kwa njia ya kipekee, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya kifedha kwa wateja wetu. Takwimu zinaonyesha kuwa sekta hii inachangia karibu asilimia 30 ya mapato ya taifa na katika biashara 10, 9 ni biashara zinazomilikiwa na wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati (SME), kati yao asilimia 54 ni Wanawake hivyo ni muhimu kuhakikisha tunawawezesha”.
Tangu tulipoanza rasmi programu hizi mnamo mwaka 2021, benki tayari imefikia wateja 500 wafanyabiashara wadogo wadogo (SME) na lengo la mwaka huu ni kufikia wateja 200. Matunda ya kile tunachofanya yanaonyeshwa katika matokeo mazuri tunayoshuhudia, ambapo faida ya benki imeongezeka kwa asilimia 33 kutoka Tsh 6.03 Bilioni hadi Tsh 9 Bilioni, kwa kulinganisha matokeo ya Juni mwaka jana na Juni mwaka huu.” alisema Cherkaoui.
Naibu Mkurugenzi Mkuu aliongeza kuwa “Benki pia imeweza kupata matokeo mazuri katika mikopo chechefu, na katika kipindi kilichofikia Juni benki imefikia asilimia 1.5 ya mikopo chechefu, hii ni chini ya kiwango kinachohitajika na Benki Kuu ya Tanzania cha asilimia 5.” Matokeo haya yanadhihirisha kuwa wateja wetu ni wazuri na wanalipa mikopo yao vizuri.”
“Ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa wateja wetu wote wa Bank of Africa Tanzania kwa kuendelea kutuunga mkono na pia naomba kwa wajasiriamali wa Tanzania, hasa wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati ((SME); benki iko tayari kuhakikisha mafanikio yao, kama kauli mbiu ya programu yetu “TUKUE PAMOJA” benki ina azma ya kuendelea kuwekeza katika sekta hii. Hii inaelezewa kwa uwazi katika mpango wa kimkakati wa miaka mitatu wa benki yetu, ukiwa na bajeti ya Tsh 62.23 Bilioni iliyopangwa kwa sekta ya wafanyabiashara wadogo wadogo na wa kati (SME) pekee kwa mwaka 2022-2024, na kwa kipindi cha mwaka jana tumetoa mikopo ya takriban Tsh 50 bilioni, huku karibia nusu yake tayari zikiwa zimekopeshwa mwaka huu hadi Juni, zikifaidisha zaidi ya wateja 16,000 wa SME.” alisema Bw. Cherkaoui.
Kaimu Mkuu wa Huduma za Kibenki kwa wateja wa reja reja (Retail Banking), Bi. Mwamvua Majeshi aliwahakikishia wafanyabiashara kwamba huduma za mikopo zitatolewa kwa wakati bila kuchelewa kulingana na kanuni za kibenki hapa nchini. Pia tunawapatia ushauri.
Alisema “Benki imefanikisha kutoa mikopo kwa biashara za kati (SMEs) yenye thamani ya shilingi bilioni 5 ikiwa imewanufaisha zaidi ya wafanyabiashara 2,000 wilayani Kahama hadi kufikia mwezi June mwaka huu”.
“Kwa Bank of Africa, wateja wetu hupata huduma kupitia matawi yetu, hata hivyo, benki pia imewekeza katika huduma za kidijitali kama vile huduma za benki kwa simu (B-Mobile), huduma za benki za mtandao (BOAWeb-Internet Banking) na hivi karibuni tumezindua huduma ya Bank of Africa WAKALA yenye mawakala zaidi ya 200 nchini na hivi karibuni itakuja na huduma ya Lipa.” alisema Bi. Majeshi.
Baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria programu hiyo waliipongeza BANK OF AFRICA kwa jinsi ilivyo wawezesha kupitia mikopo na kuinua biashara zao na kuomba benki iendelee kuboresha huduma zake ili kufaidisha Watanzania wengi zaidi.