Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) limeanza msimu wa nne wa kampeni ya “Twenzetu Kileleni” safari inayolenga kuimarisha utalii wa ndani kwa kuhamasisha Watanzania zaidi kupanda Mlima Kilimanjaro. Badala ya kutegemea tu wageni wa kimataifa, kampeni hii inawalenga Watanzania wenyewe, ikiwapa fursa ya kutembelea moja ya maajabu ya asili ya dunia, huku ikiimarisha uzalendo wa kitaifa.
Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara TANAPA, Jully Lyimo, kampeni hii ni zaidi ya utalii. Inatoa nafasi kwa Watanzania kuungana na urithi wa taifa lao, huku wakiadhimisha siku ya Uhuru wa Tanganyika kwa njia ya kipekee. “Hii siyo tu safari ya utalii, bali ni ishara ya uzalendo na urithi wetu wa kihistoria. Tangu mwaka 1961, Watanzania wamekuwa wakipanda mlima huu kama sehemu ya kuadhimisha uhuru wetu, na tunataka kuendeleza utamaduni huo,” alisema Lyimo.
Msimu huu wa nne unaambatana na kauli mbiu: “Stawisha Uoto wa Asili, Okoa Barafu ya Mlima Kilimanjaro”, ikilenga kuhamasisha umuhimu wa kulinda mazingira na uoto wa asili unaozunguka mlima. Hili limekuja wakati ambapo barafu la kilele cha Kilimanjaro linazidi kupungua kwa kasi, huku mabadiliko ya tabianchi yakiwa ni tishio kubwa kwa vivutio hivi vya asili. Kupitia kampeni hii, TANAPA inatarajia Watanzania wengi zaidi watashiriki si tu kama watalii, bali pia kama mabalozi wa mazingira.
Mapinduzi Mdesa, Ofisa Uhifadhi Mkuu wa TANAPA, alieleza kuwa kampeni hii inatoa nafasi kwa washiriki kugundua vivutio mbalimbali vilivyomo katika maeneo ya Mlima Kilimanjaro, kama vile maporomoko ya maji na mandhari za kipekee ambazo wengi hawajaziona. “Sio tu kupanda mlima, lakini pia tunataka washiriki wafurahie safari yenyewe, waone yale ambayo huenda hawakuwahi kuyashuhudia,” alisema.
Lakini kampeni hii imechukua sura mpya mwaka huu, kwani imejumuisha pia michezo na shughuli za kiutalii kama vile kupandisha parachute, mpira wa miguu kwenye uwanja wa juu kabisa, na mbio za baiskeli. TANAPA inaongeza ubunifu wa namna ya kufanya utalii huu uvutie zaidi kwa Watanzania, na kuendelea kuwavutia wageni wa ndani pamoja na wale wa nje.
Faustin Chombo, muongoza wageni kutoka kampuni ya utalii ya ZARA, alionyesha shukrani kwa serikali kwa kuendeleza juhudi hizi za kukuza utalii wa ndani. Alisema kuwa mwaka jana waliona ongezeko la watalii wa ndani, na mwaka huu wanatarajia namba hiyo kuongezeka zaidi kutokana na mwamko huu mpya.
Kupanda Mlima Kilimanjaro kwa sasa sio tu ndoto ya wageni kutoka mataifa ya mbali, bali ni nafasi kwa Watanzania kuupanda mlima wao wenyewe, kujivunia urithi wao, na kusaidia juhudi za kuhifadhi uoto wa asili na mazingira ya Tanzania kwa ujumla.